Habari

Jubilee yachafua Katiba

August 2nd, 2020 3 min read

Na MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Rais Uhuru Kenyatta inaendelea kulaumiwa kwa kutotilia maanani hitaji la kuheshimu Katiba kikamilifu, huku taifa likiingia katika mwezi wa kuadhimisha mwongo mmoja tangu Katiba ya sasa ilipopitishwa na kuidhinishwa.

Mnamo Agosti 4, 2010, wananchi walipigia kura Katiba ya sasa kwa wingi wakitumai italeta mabadiliko, kisha ikaidhinishwa Agosti 27 chini ya utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Lakini sasa, wadadisi na wataalamu wa kisheria wanasema kuna mambo mengi hayajatimizwa na mengine yakipuuzwa.

Rais Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga wanatarajia kufanyia marekebisho katiba hiyo kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mojawapo ya masuala makuu ambayo yamefanya utawala wa Rais Kenyatta kuonekana kutojitolea kuheshimu Katiba ni jinsi bunge la Taifa na Seneti zilivyoshikwa mateka na Ikulu.

Kikatiba, vitengo hivyo viwili vya serikali vinafaa kuwa huru kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa na asasi za nje.

Hata hivyo, matukio ya tangu 2013 hadi sasa yanaonyesha hali tofauti, kwani baadhi ya sera na sheria zinazopitishwa ni kwa msingi wa matakwa ya Afisi ya Rais.

Kulingana na Mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri, adhabu inayotolewa kwa wakosoaji wa serikali bungeni ni ishara tosha ya jinsi Katiba inavyopuuzwa chini ya utawala wa Jubilee.

“Nataka kuwaambia Wakenya kuwa hakuna Seneti wala Bunge mpaka tuchaguane 2022,” akasema alipozungumza jana katika eneo la Kapsaret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Ni hali hii ambayo ilifanya wengi kushangaa wiki iliyopita, wakati maseneta walipokataa kufuata amri ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhusu mfumo mpya wa ugavi wa fedha za kaunti. Kimsingi, ilitarajiwa maseneta wangeendeleza mtindo wa kuimba wimbo wa vigogo hao wa kisiasa.

BUNGE KUTEKWA

Thibitisho la jinsi bunge lilivyotekwa lilionekana wazi pia hivi majuzi, wakati Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, alisema mbunge yeyote anayetaka kuepuka adhabu anafaa kufuata masharti ya vigogo Rais Kenyatta na Bw Odinga “kama ng’ombe”.

Alisema hayo wakati wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, ambao ndio sasa wanaonekana kuwa wa upande wa upinzani, walipoadhibiwa kwa misimamo yao inayoenda kinyume na matakwa ya Rais.

Kando na Afisi ya Rais na Bunge, kikatiba kitengo cha tatu huru cha serikali kinafaa kuwa Mahakama.

Kwa kuzingatia matamshi ya Jaji Mkuu David Maraga mara kwa mara, ishara zinaonyesha kumekuwepo juhudi za kuvuruga uhuru wa kitengo hicho.

“Kunafaa kuwepo vitengo vitatu vya serikali. Wameua bunge, mahakama na sasa kilichobaki ni udikteta. Hata mimi nikiongea saa hii nitapata bunduki yangu imeenda, walinzi wamechukuliwa…hii ni aibu,” akaeleza Bw Ngunjiri.

Katika hotuba zake kuhusu hali ya mahakama, Jaji Maraga, ambaye ndiye Rais wa Mahakama, huwa hafichi mahangaiko anayopitia chini ya utawala wa Rais Kenyatta.

Yeye hulalamikia changamoto kama vile kunyimwa fedha za kutosha kusimamia idara hiyo, na uamuzi wa Afisi ya Rais kutoheshimu maagizo ya korti.

Agizo la hivi majuzi ambalo limeendelea kughadhabisha Mahakama ni kuhusu uamuzi wa Rais kukataa kuapisha majaji 41 licha ya kuagizwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki alidai serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Serikali Kuu pia hulaumiwa kwa kukiuka maagizo mengine ya korti ikiwemo kutofurusha watu katika ardhi zao.

KUPUUZA MAAGIZO YA KORTI

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i, alishikilia kwamba polisi hawatatii agizo lolote la mahakama bila kupata idhini kutoka kwa Mwanasheria Mkuu.

“Tutaheshimu maagizo ya mahakama mradi tu yawe yameidhinishwa na Mwanasheria Mkuu,” akasema.

Kando na haya, uamuzi wa Rais Kenyatta ‘kumeza’ vyama vya upinzani na kumefanya demokrasia kuwa hafifu.

Vyama vikuu vya upinzani vilivyomezwa ni ODM na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka.

Wakosoaji wa mpango huu wasema kuwa umeasi siasa ya vyama vingi ambayo ni muhimu kwa ukuzaji demokrasia nchini.

Kando na haya, malalamishi ya magavana kuhusu ugavi wa fedha hutajwa kama mbinu ya serikali kuu kulemaza ugatuzi.

Kulingana na Tume ya Kimataifa ya Mawakili, ugatuzi ulikuwa mojawapo ya vigezo muhimu kwa Wakenya kupitisha Katiba kwani walitarajia kuletewa uongozi karibu nao ili kuwe na usawa kimaendeleo.

“Afisi ya Rais inafaa kutekeleza Katiba kikamilifu hasa kuhusu ugatuzi. Inafaa kuheshimu malengo ya ugatuzi na kuhakikisha ugavi wa fedha unafanywa kwa usawa, na serikali kuu isidunishe majukumu ya serikali za kaunti kwa kuchelewesha kutuma fedha mashinani,” Mwenyekiti wa ICJ, Bw Kelvin Mogeni anaeleza.

Katika masuala ya ugatuzi, serikali ya Rais Kenyatta imelaumiwa pia kwa jinsi ilivyotwaa baadhi ya majukumu ya kusimamia Kaunti ya Nairobi.