Habari

Jubilee yaelezea uwezekano wa kumwadhibu Kamanda

September 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Maalum Maina Kamanda amejipata kwenye kikaangio kwa kuunga mkono mgombea wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra badala ya mgombea wa Jubilee, McDonald Mariga.

Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amesema kuwa Bw Kamanda ataadhiniwa “baada ya uongozi wa chama kufanya mashauriano na kamati ya nidhamu kuhusu ukiukaji huo wa sheria za chama.”

“Sheria za chama zinapasa kuzingatiwa. Kwa hivyo, hatua ya kuunga mkono mgombeaji wa chama kingine wakati ambapo chama chetu kina mgombeaji katika uchaguzi ni makosa. Nashauriana na kamati ya nidhamu kuhusu hatua ambayo inapasa kuchukuliwa,” Bw Tuju akasema.

Mnamo Alhamisi Bw Kamanda ambaye zamani alikuwa mbunge wa Starehe alimtembelea kiongozi wa ODM afisini mwaka, jumba la Capitol Hill, Nairobi ambapo alitangaza hadhari ni anamuunga Benard Imran Okoth.

Hata hivyo, alisema amechukua hatua hiyo kwa sababu ya handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga ambayo imeleta utulivu nchini tangu mwaka jana.

“Namuunga mkono Imra Okoth kwa sababu amani ambayo tunafurahia nchini kutokana na handisheki, haswa hapa Nairobi. Ninamuunga mkono kama mtu binafsi,” akasema Bw Kamanda.

Alitoa tangazo hilo siku moja baada ya Rais Kenyatta kumwidhinisha rasmi Bw Mariga kama mgombeaji wa Jubilee katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi.

“Natangaza kuwa nakuunga mkono na ninakutaki ushindi katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Kibra,” Rais akasema kabla ya kumvisha Bw Mariga kufia nyekundu ya Jubilee.

Kukaidi

Hatua ya Kamanda ya kumuunga mkono Imran Okoth iliwakera viongozi wa Jubilee waliosema ni ishara ya kukaidi chama ambacho kilimteua bungeni.

“Kamanda anafaa kujiuzulu sio tu wadhifa wake kama Mbunge bali hafai kuendelea kuwa mwanachama wa Jubilee. Ni kinyume cha sheria za vyama vya kisiasa na Katiba kwa mwanachama wa chama kimoja kuunga chama pinzani bila kujiuzulu kwanza,” akasema Mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome.

Lakini Jumamosi, Mbunge wa Nyeri Mjini alimtetea Kamanda akisema hafai kuadhibiwa kwa misingi ya kuunga mkono mgombeaji wa ODM.

“Viongozi wengine wamewahi kukaidi chama na ajenda zake lakini hatujawahi kusikia wanaadhibiwa. Mmoja wao ni William Ruto mwenyewe ambaye anapinga handisheki na vita dhidi ya ufisadi,” akasema.

“Ikiwa ni kuadhibiwa upanga huo unapasa kukata pande zote,” akaongeza Bw Wambugu.

Kando na Bw Kamanda, viongozi wengi wa Jubilee ambao wameahidi kuunga mkono mgombeaji wa ODM ni; seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.