Habari Mseto

Jubilee yakanganya Ruto kuhusu ODM kujiondoa

April 11th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee Jumatano kiliiondolea ODM aibu kilipothibitisha kuwa chama hicho kilijiondoa kutoka uchaguzi mdogo wa Wajir Magharibi, kufuatia makubaliano na uongozi wa vyama hivyo viwili.

Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, Katibu Mkuu Raphael Tuju, alisema hatua hiyo ililenga kupunguza joto la kisiasa nchini, ili kutoa nafasi kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupalilia maridhiano.

“Kujiondoa kwa ODM kunatokana na mashauriano, na makubaliano, kati ya safu ya juu ya uongozi wa vyama hivi viwili. Mashauriano sawa na hayo yalifanya Jubilee kutowasilisha wagombeaji katika chaguzi ndogo za Migori, Ugenya na Embakasi Kusini,” akasema Bw Tuju.

Kauli ya Jubilee inakinzana na kauli iliyotolewa na Naibu Rais William Ruto mnamo Jumanne, kwamba ODM ilijiondoa kutoka kinyang’anyiro hicho baada ya mgombeaji wake Prof Mohamed Yusuf Elmi kujiunga na chama cha Jubilee.

Kwenye taarifa iliyotumwa na kitengo cha habari za naibu rais (DPPS), Prof Elmi alihama ODM baada ya kushauriwa na viongozi na wazee wa ukoo wake wa Degodia.

Kabla ya taarifa ya Prof Elmi, ODM ilikuwa imetangaza kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa kile ilichosema ni katika moyo wa handisheki.

Taarifa hii inafanana na ile iliyotolewa na Bw Tuju, lakini inatofautiana na ile iliyotolewa na Dkt Ruto.

Lakini wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na kiongozi wa wengi bungeni, Bw Aden Duale, walisema ODM ilijiondoa kutoka uchaguzi huo mdogo ili kuzuia aibu ya kushindwa tena sawa na ilivyofanyika katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini.