HabariSiasa

Jubilee yakiri Cambridge Analytica iliwasaidia uchaguzini 2017

March 21st, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha Jubilee kimekiri kusaidiwa na kampuni ya Strategic Communications Laboratory (SCL) inayohusishwa na Cambridge Analytica (CA) inayotambuliwa kwa uenezaji wa propaganda hasa katika uchaguzi.

Hata hivyo, chama hicho kimekiri kulipa kampuni hiyo kwa huduma zake za kupatia chama sura ya kipekee -“branding” katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Cambridge Analytica (CA), inakabiliwa na kashfa ya kutumia hila katika uchaguzi ambayo inahusisha Facebook.

Habari hizo zimegonga vichwa vya habari kufuatia mahojiano yaliyorekodiwa ambapo wakuu wake walielezea wajibu wao katika mkondo ambao uchaguzi wa 2013 na 2017 ulichukua, kupitia propaganda kali za kuwagawanya watu na pia ukabila mtandaoni.

Kulingana na taarifa za maafisa hao zilizorekodiwa kisiri na kipindi cha British Channel 4 kilichoonyeshwa Jumatatu, CA ambayo ilitambulika mara ya kwanza kwa kuhusika kwake katika kampeni ya urais wa Donald Trump 2016, pia iliendesha kampeni za Rais Uhuru Kenyatta 2013 na 2017.

Lakini naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, alipuuzilia mbali kuhusika kwa kampuni hiyo kwa njia kubwa, akisema tu kuwa ilihusika zaidi na huduma za kuiunda sura yake.

 

Jubilee yabana maelezo

Hata hivyo, Bw Murathe hakutoa maelezo zaidi kuhusu kile kampuni ya Cambridge inayohusika na SCL ilifanyia chama cha Jubilee nchini.

Chama cha ODM sasa kinawataka wakuu wa Jubilee kujitokeza na kuweka wazi mchango wa CA katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliopita.

“Katika moyo wa mazungumzo ulioanzishwa na vinara wetu wawili, tungependa Jubilee iweke wazi ushirikiano wake na CA ili tuweze kukabiliana na ushawishi wa kisiasa kutoka nje katika siku sijazo na kulinda demokrasia yetu kama nchi,” alisema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Katika kanda hiyo ya Channel 4 News, meneja Mkurugenzi wa Cambridge Analytica na SCL Elections, amenaswa kwa video akijigamba jinsi kampuni hizo zilivyohusika katika uchaguzi wa Kenya wa 2013 na 2017.

Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Reuters, Cambridge Analytica imekana madai yaliyotolewa na Channel 4 News, ikisema iliwaelekeza wanahabari hao wapekuzi kwa lengo la kujua nia yao.

 

Uchunguzi

Kwa sasa, afisi zake za London zinatarajiwa kuchunguzwa huku kukiwa na maswali pia kutoka kwa wakuu wa Amerika baada ya mfichuzi kueleza jinsi kampuni ilivyosaka habari za kibinafsi za mamilioni ya watu kwa lengo la kusaidia kampeni ya Rais Trump.

Taarifa hizo za kuhusika kwa kampuni hiyo ya Uingereza zimeibua hisia mseto nchini Kenya.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen (Jubilee), alikanusha taarifa kuwa kampuni hizo zilishawishi jinsi uchaguzi ulivyofanyika.

Wakati huohuo aliyefichua sakata ya CA, Christopher Wylie alisema mwenzake alipatikana amekufa katika hoteli moja nchini Kenya.

Alisema Dan Muresan, aliyedaiwa kushiriki katika kampeni za Rais Kenyatta wakati wa uchaguzi wa 2013 alipatikana amekufa katika hali isiyoeleweka.