Habari

Jubilee yaadhibu Maraga?

October 30th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Serikali kupunguza bajeti ya Mahakama imesababisha hisia kali huku wengi wakiitaja kama kutimiza vitisho alivyotoa Rais Uhuru Kenyatta Mahakama ya Juu ilipofuta ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Huduma katika mahakama kote nchini ziliathiriwa na hatua hiyo kufuatia uhaba wa pesa na majaji na juhudi za kupunguza mrundiko wa kesi zilisitishwa.

Hii ni licha ya serikali kulaumu mahakama kwa kuchukua muda mrefu kuamua kesi.

Akihutubia wafuasi wa Jubilee katika eneo la Burma, Nairobi muda mfupi baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wake kwenye uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Rais Kenyatta aliwataja majaji kama wakora na akaapa kurejelea suala hilo akishinda marudio ya uchaguzi huo.

“Wajua uzuri wa sheria, hapo awali nilikua rais mtarajiwa, si ni kweli? Si Maraga na hao watu wake wakora wamesema basi uchaguzi ipotee? Si ndivyo wamesema? Sasa mimi tena sio mtarajiwa! Mimi ni Rais ambaye amekalia kiti. Sijui kama mnaelewa? Maraga ajue ya kwamba sasa ana-deal (anakabiliana) na Rais anakalia kiti,” Rais Kenyatta alisema na kuongeza kwa Kiingereza: “We shall revisit”(Tutarejelea suala hili).”

Katika kipindi chake cha pili uongozini, Rais Kenyatta kila anapopata nafasi, huwa hasiti kulaumu Mahakama kwa kulemaza ajenda za serikali yake kupitia majaji anaodai wanashirikiana na wanaharakati na wafanyabiashara.

Ikizingatiwa kuwa serikali ilipunguza bajeti ya idara na mashirika muhimu ya serikali kufadhili Ajenda Nne Kuu za serikali, Wakenya wanasema analenga kuikata miguu ili Mahakama isiwe na uwezo wa kukanyagia breki miradi yake.

Aidha, amekuwa akiilaumu kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi. Hisia za wengi ni kwamba, alianza kutimiza ahadi yake ya kunyorosha mahakama, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alipokamatwa kwa madai ya kutumia vibaya mamlaka na kuhusika na ufisadi.

Jaji Mwilu aliokolewa na Mahakama iliyokosoa mbinu ambazo wapelelezi walitumia kupata ushahidi wa kumfungulia mashtaka.

Wakitoa hisia zao kwenye mitandao, Wakenya walisema serikali ilianza kuandama mahakama Jaji Mwilu aliposhtakiwa.

“Si Rais Kenyatta aliahidi kukabiliana na mahakama? Hii inahusisha hatua kama kupunguza bajeti na kukataa kuchapisha majina ya majaji 41,” aliandika Jerotich Seii kwenye Twitter.

Kulingana na wakili Nelson Havi, chanzo cha masaibu ya Jaji Mwilu ni vitisho walivyotoa viongozi wa Jubilee baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha ushindi wao.

Mwaka 2018 alikawia kuchapisha jina la Jaji Mohammed Warsame kuwa kamishna wa Tume ya Mahakama (JSC) akisema, hakuwa amepigwa msasa inavyohitajika kisheria hadi Mahakama ilipotoa agizo uteuzi wake utekelezwe.

Mwaka 2019 amekataa kuchapisha majina ya majaji 41 waliopandishwa vyeo akisema ana habari kwamba maadili yao ni ya kutiliwa shaka.

Ikizingatiwa kuwa Rais anawakilishwa katika JSC na Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki na wawakilishi wengine watatu waliopitisha majina ya majaji hao, sababu zake kukataa kuchapisha majina yao hazijaridhisha wengi.

Japo kwenye bajeti ya mwaka 2019 Mahakama ilikuwa imeomba Sh31.2 bilioni, ilitengewa Sh17.3 bilioni pekee ambazo sasa zimepunguzwa zaidi kwa Sh3 bilioni hadi ikalazimika kusitisha mahakama za kuhamahama na majopo yanayosikiliza na kutatua mizozo mbali mbali. Kulingana na wakili Ahmednasir Abdullahi, hatua ya serikali itazamisha mahakama zaidi kuliko ilivyofanya serikali ya Kanu.

“Mahakama nyingi zitafungwa ifikapo Desemba. Nasikia Mahakama ya Rufaa itazama kwa asilimia 70 ifikapo Desemba, hata Kanu ilielewa vyema umuhimu wa kuwa na mahakama inayotekeleza majukumu yake kuliko Jubilee,” alisema Bw Abdullahi.

Baadhi ya majopokazi yaliyoathiriwa yanahusika na mizozo inayoweza kuzuka kutokana na utekelezaji wa Ajenda Nne za serikali kama ile ya kushughulika na mazingira na ardhi.

“Ukweli ni kwamba, mfumo wa mahakama nchini umevurugika na serikali ndiyo ya kulaumiwa,” alisema wakili huyo.

Hatua hii imefanya Mahakama kusimamisha marupurupu kwa majaji na wafanyakazi wote.

Mwakilishi wa chama cha wanasheria katika JSC Macharia Njeru pia alikosoa kupunguzwa kwa bajeti ya mahakama. Chama hicho kimeshtaki Wizara ya Fedha kwa hatua hiyo.