Habari Mseto

Jubilee yapanga kuwaadhibu wabunge kutoka Mlima Kenya wanaoonekana kuunga azma ya Ruto

May 10th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee kinapanga kuwaadhibu wabunge wa mrengo unaohusishwa na kuunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais mwaka 2022 na hivyo kuonekana kukaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba wasitishe kampeni za mapema.

Baadhi ya vyombo vya habarui nchini Kenya vimekuwa na mazoea ya kuwaita ‘Tanga Tanga’.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba katika mkutano uliofanyika Alhamisi na kuhudhuriwa na maafisa fulani wa serikali, iliafikiwa kuwa wabunge hao wapokonywe nafasi wanazoshikilia katika kamati za bunge zenye mamlaka makuu.

Wanaolengwa ni pamoja na Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa na Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata ambaye ni naibu kiranja wa wengi katika seneti.

Wengine ni Seneta wa Nakuru, Susan Kihika ambaye pia ni kiranja wa wengi katika seneti na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Sabina Wanjiru Chege ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya.

Pia inasemekana kuwa teuzi za hivi majuzi za wanasiasa ambao walishindwa na wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto haswa kutoka eneo la Mlima Kenya ni sehemu ya mpango mpango wa kuwaadhibu wabunge hao waasi.

Kwa mfano katika eneo la Murang’a wapinzani wa wabunge wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu waliteuliwa katika mashirika ya serikali.

Na wale wabunge wa mrengo wa ‘Kieleweke’ –  yaani wanaopinga ndoto za Dkt Ruto ya kumrithi Rais Kenyatta hawakuguswa.

Wapinzani wapewa kazi

Katika maeneobunge ya Maragua, Kiharu na Kandara, wapinzani wa wabunge wa sasa walipewa kazi serikalini.

Elius Mbau aliyeshindwa na Mary Waithira katika eneo bunge la Maragua katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya shirika la NEPAD, Joshua Toro aliyebwagwa na Alice Wahome kule Kandata aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kitaifa la Unyunyiziaji (NIB).

Na mwanasiasa Karanja Mburu aliyeshindwa na Ndindi Nyoro kule Kiharu aliteuliwa kuwa mwanachama wa bodi ya mradi wa LAPSSET.