Habari

Jubilee yaruka Mariga katika Kibra

August 28th, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Jubilee kimekanusha kwamba kiliorodhesha jina la mwanasoka wa kimataifa MacDonald Mariga miongoni mwa wanaotaka tiketi yake ili kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Kibra hapo Novemba 7.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alikanusha Jumanne kwamba aliandika barua yenye jina la Bw Mariga na watu wengine wanne huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikikataa barua hiyo na kuirudisha kwa usimamizi wa Jubilee.

Mwanasoka huyo pamoja na ndugu yake Victor Wanyama waligonga vichwa vya habari nchini mwezi jana baada ya kumtembelea Naibu Rais William Ruto katika ofisi yake wakati wa kupanga mashindano ya soka ya Wanyama Royal Cup yanayodhaminiwa na wawili hao.

Ni kutokana ziara hiyo ambapo barua iliyoorodhesha jina la Bw Mariga ilionekana na wengi kuwa azma yake ya kuwa mbunge wa Kibra inapigwa jeki na Dkt Ruto.

Wengine waliotajwa kama wanaomezea mate kiti cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee kwenye barua hiyo tatanishi ni Said Abraham, Morris Peter Kinyanjui, Mukinyingi Walter Trenk na Doreen Nangame Khayanga Wasike.

“Tume ilipokea barua Jumatatu Agosti 26 saa kumi na moja jioni ikipendekeza majina ya wawaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra. Hata hivyo, tume imeelezwa kwamba Jubilee haikuidhinisha barua hiyo. Tume imeandikia chama na kuambatanisha nakala ya barua hiyo ili chama kichukue hatua inayofaa,” ikasema taarifa ya IEBC.

Bw Tuju mnamo Jumatatu jioni alieleza kutofahamu lolote kuhusu barua hiyo iliyochipuka punde tu baada yake kutoa taarifa kwamba chama hicho kitawasilisha mwaniaji kuchuana na mgombeaji wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga ili kutafuta mrithi wa marehemu Ken Okoth.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Dijitali katika Afisi ya Rais, Dennis Itumbi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusambaza barua hiyo na kusema ilikuwa na saini ya Bw Tuju kama thibitisho kwamba aliidhinisha.

“Nasimama na barua niliyosambaza kuhusiana na uchaguzi wa Kibra. Jubilee itaandaa kura ya mchujo. IEBC ina barua ambayo nimeambatanisha hapa,” akaandika Itumbi kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mchujo

Huku hayo yakijiri, Bw Tuju alikanusha kwamba chama hicho kitafanya kura ya mchujo, akisema wenye nia ya kutumia Jubilee kupigania kiti cha Kibra watakaokuwa wamewasilisha vyeti vyao watachujwa Ijumaa hii kisha uamuzi wa mgombeaji wa kupewa tiketi ya moja kwa moja uafikiwe na chama.

Wakati huo huo Bw Tuju alieleza Taifa Leo kwamba hatua ya chama hicho kumwasilisha mwaniaji kukabiliana na ODM Kibra haitavuruga ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga maarufu kama handisheki.