Habari

Jubilee yasaliti Kibaki

October 11th, 2019 4 min read

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI ya Jubilee imemsaliti Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa kupuuza sera zake za kiuchumi zilizosaidia kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida.

Kutokana na usaliti huo, maisha ya mwananchi wa kawaida yameendelea kuwa magumu kinyume na yalivyokuwa yameimarika wakati wa utawala wa mbunge huyo wa zamani wa Othaya.

Wananchi waliohojiwa na Taifa Leo maeneo mbalimbali ya nchi walieleza kuvunjika moyo kutokana na gharama ya juu ya maisha, ongezeko la umaskini, uhaba wa nafasi za kazi, hali ya kuchanganyikiwa katika sekta ya elimu, huduma duni za hospitali na ukosefu wa mikopo ya kujistawisha kibiashara.

Alipokuwa akikabidhi mamlaka kwa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto mnamo 2013, Mzee Kibaki aliwaambia: “Ninawaachia nchi iliyo tayari kupaa katika ustawi, usawa na umoja. Tunapaswa kulenga darubini yetu katika kujenga Kenya bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Deni kubwa

Wadadisi wa masuala ya uchumi na utawala wanasema kwamba badala ya kuendeleza sera za Mzee Kibaki zilizofanya Kenya kufanikiwa kufadhili asilimia 95 ya bajeti bila kutegemea mikopo ghali, serikali ya Jubilee iliamua kutegemea madeni hasa ya kigeni na katika kipindi cha miaka mitano cha utawala wao Kenya ilikuwa ikidaiwa zaidi Sh5.8 trilioni.

Mzee Kibaki alipoondoka madarakani Kenya ilikuwa na deni la Sh1.6 trilioni, ambapo Sh 527 bilioni zilikopwa mashirika ya fedha ya humu nchini.

Mnamo Jumatano, Bunge liliipatia serikali idhini ya kuongeza madeni hadi Sh9 trilioni licha ya mashirika ya wafadhili kuonya kuwa madeni ya Kenya yamevuka mipaka.

Mwanauchumi David Ndii anakosoa sera za serikali ya Jubilee akisema haziwezi kukuza uchumi mbali zinasaidia tu kampuni chache zinazomirikiwa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Sera za serikali ya Mzee Kibaki zilikuwa halisi na utekelezaji wake ulikuwa ukibainika wazi na zililenga kupunguzia mwananchi wa kawaida gharama ya maisha na kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini.

Mabwanyenye

Wadadisi wanaeleza kuwa kinyume na utawala wa Mzee Kibaki ambao nia yake kuu ilikuwa kusaidia mwananchi wa kawaida, utawala wa Jubilee unajishughulisha zaidi kufaidi mabwanyenye kibiashara.

“Mipango ya maendeleo ya Jubilee huzingatia zaidi ni nani katika serikali ambaye atanufaika kibiashara. Ingawa hata wakati wa Kibaki baadhi ya maafisa wake walikuwa na tabia hii, hali imekuwa mbaya zaidi sasa,” akasema mdadisi mmoja.

Baadhi ya sera za uchumi za serikali ya Jubilee zimerudisha Kenya nyuma huku wawekezaji waliokuwa na imani na nchi hii wakihamia mataifa mengine, tofauti na ilivyokuwa chini ya utawala wa Mzee Kibaki.

Chini ya utawala wa Mzee Kibaki, kampuni zilikuwa zikipata faida kubwa, kupanua shughuli na kuajiri idadi kubwa ya Wakenya. Lakini kwa wakati huu nyingi zinatangaza hasara, kufuta wafanyakazi, kufungwa ama kuhamia mataifa mengine kama Misri, Tanzania na Ethiopia.

Wananchi waliohijiwa na Taifa Leo walisema Jubilee inatoa sera ambazo hazifaidi mwananchi wa kawaida licha ya serikali kushinikiza zitekelezwe.

“Kwa mfano unashangaa nia ya kuagiza mizigo yote isafirishwe kwa SGR. Hii inamaanisha serikali haitujali sisi tuliowekeza katika sekta ya uchukuzi,” akasema mmiliki wa kampuni moja ya mizigo jijini Mombasa.

Kupitia sera za utawala wa Mzee Kibaki, sekta ya fedha ilistawi na benki zikaanza kutoa mikopo nafuu kwa Wakenya wa kawaida kuendeleza biashara.

“Nakumbuka benki zilikuwa zikiwasihi wananchi kuchukua mikopo. Siku hizi ni vigumu sana kwa mwananchi wa kawaida kupata mkopo wa benki,” akasema Anderson Kimani ambaye ni mfanyibiashara Nairobi.

“Hatua hii ilifanya kuwepo kwa pesa nyingi za uzalishaji na biashara, hali ambayo ilichochea ukuaji wa uchumi,” asema mdadisi wa masuala ya uchumi David Kimotho.

Sera bora

Wadadisi wanasema kama serikali ya Jubilee ingeendeleza sera za uchumi za utawala wa Mzee Kibaki, uchumi ungekuwa thabiti zaidi na Kenya haingekuwa na mlima wa madeni.

“Inasikitisha kuwa licha ya utawala wa Mzee Kibaki kupata mafanikio makubwa ya kuboresha maisha ya Wakenya, hatuwasikii viongozi wa Jubilee wakienda kumuomba ushauri,” Janet Mumbua kutoka Kajiado alieleza Taifa Leo kwenye mahojiano.

Ingawa wadadisi wanasema uchumi wa Kenya ulikua vyema katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Jubilee kutoka 2013 hadi 2017, wanasema hii ilikuwa ni matokeo ya sera za Mzee Kibaki.

Chini ya utawala wa Jubilee kodi ziliongezeka na mpya kuanzisha kwa lengo la kupata pesa za kulipa madeni hasa ya China, jambo lililofanya gharama ya maisha kwa mwananchi wa kawaida kupanda.

“Kodi mpya zimechangia mfumko wa gharama ya maisha. Uwezo wa Wakenya wa kununua bidhaa na huduma umepungua tofauti na ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mzee Kibaki ambapo sekta kama ya ujenzi ilistawi,” alikiri mwanauchumi mmoja wa serikali.

Wananchi walia

Tofauti na utawala wa Kibaki ambao ulipanua sekta ya elimu kwa kuanzisha elimu bila malipo na kupanua vyuo vikuu nchini, sekta ya elimu kwa sasa inakumbwa na matatizo mengi ikiwemo utekelezaji wa mfumo wa elimu wa CBC.

Japo utafiti wa kubadilisha mfumo wa elimu ulifanywa chini ya utawala wa serikali ya Mzee Kibaki, haikuwa na haraka ya kutekeleza mabadiliko hayo bila kuweka msingi unaohitajika.

Hali ni sawa katika sekta ya kilimo ambapo wakulima wanalia wamepuuzwa.

Alipoingia mamlakani 2003, Mzee Kibaki aliwekeza Sh6.4 bilioni katika sekta ya majanichai na Sh2.5 bilioni sekta ya kahawa ili kuokoa wakulima kutokana na madeni. Hatua hii ilifanya wakulima kupanua kilimo cha majanichai kutoka hektari 131,500 hadi 187,855 kufikia 2011.

Chini ya utawala wa Jubilee wakulima wameanza kung’oa majanichai huku kampuni kubwa zikihamia mataifa jirani ya Afrika Mashariki zikilalamikia sera mbaya na viwango vya juu vya kodi.

Mnamo 2013, serikali iliwanunulia wakulima wa mahindi gunia moja kwa Sh3,000 lakini chini ya utawala wa Jubilee serikali ilitangaza bei ya Sh2,300 kwa gunia la kilo 90 licha ya kuwa gharama za uzalishaji zimepanda tangu 2013.

Hata hivyo Jubilee imeendelea kutekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na Mzee Kibaki kama SGR, Bandari ya Lamu na ujenzi wa barabara kote nchini. Lakini kumekuwa na malalamiko ya gharama kuongezeka pamoja na kutegemea mikopo ya kigeni kuifadhili.