Habari

Jubilee yataka IEBC imfungie nje mgombea wa ODM Kibra

October 14th, 2019 2 min read

Na COLLINS OMULO

KAMPENI za uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra zinazidi kuchukua mkondo wa kutisha, kwani wanasiasa wanaonekana kutumia propaganda zinazotishia kuchochea umma.

Pande mbili kuu pinzani katika uchaguzi huo – ambazo ni chama cha ODM na Jubilee – ndizo zinazozozana zaidi kwa maneno na vitendo ambavyo baadhi ya viongozi wanasema vinastahili kuzimwa mara moja.

Mnamo Jumamosi, gari lililokuwa kwenye msafara wa Bw McDonald Mariga anayepeperusha bendera ya Jubilee lilirushiwa mawe na kuvunjwa vioo na watu wasiojulikana.

Viongozi wa Jubilee mnamo Jumapili waliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imzuie mgombeaji wa ODM, Bw Bernard ‘Imran’ Okoth kuwania wadhifa huo kwani wanaamini shambulio hilo lilitendwa na wafuasi wa ODM.

Lakini kwa upande mwingine, wanasiasa wa ODM wanadai kisa hicho kilikuwa ni njama ya wapinzani wao kutaka Imran aondolewe kwenye kinyang’anyiro.

“Tunataka kushindana kwenye ulingo ulio na amani kwa hivyo hebu wagombeaji wote na vyama vyote vya kisiasa wakumbatie amani na kuwapa watu wa Kibra nafasi ya kujichagulia kiongozi wanayemtaka,” Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema Jumapili, akidai ODM inajaribu kuwahangaisha wasifanye kampeni huko.

Viongozi wa ODM walijitetea na kusema kuwa wanaodai kuwa Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw Simba Arati ndiye alihusika, watoe ushahidi.

“Huwezi kusema ni Arati kama huna ushahidi. ODM haikuhusika na tunaomba wafuasi wetu wafanye kampeni kwa amani,” akasema Mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Nairobi.

Madai yaliyozagaa katika eneobunge hilo wakati wa kampeni kama vile ya wanasiasa kuhonga wapigakura, vitambulisho vya wapigakura kununuliwa, na pia wapigakura kuingizwa kwenye sajili kutoka maeneobunge mengine, yamezidisha taharuki ya kisiasa eneo hilo.

Zaidi ya madai hayo, hatua ya Mbunge Maalumu wa Jubilee, Bw Maina Kamanda ambaye anapigia debe ODM, kuingiza masuala ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 katika kampeni hizo pia imeibua wasiwasi kuhusu mkondo unaochukuliwa na kampeni hizo.

Wakosoaji wa Bw Kamanda wanasema ni hatari kufufua suala hilo katika kampeni za kisiasa ilhali inafahamika wazi kuwa ukatili ulioshuhudiwa katika ghasia hizo, ulisababisha zaidi ya watu 1,100 kuuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao hadi leo.