HabariSiasa

JUBILEE YATOKOTA: Joto kali huku wandani wa Uhuru na Ruto wakikabana

June 28th, 2018 3 min read

BENSON MATHEKA Na GRACE GITAU

KUIBUKA kwa mirengo miwili mikuu ndani ya chama tawala cha Jubilee kumezua tofauti zinazotishia kuvuruga chama hicho.

Tofauti hizo zimetokana na masuala manne makuu ambayo ni: Jinsi vinavyoendeshwa vita dhidi ya ufisadi; misako ya kunasa bidhaa feki; mwafaka wa Rais Kenyatta na Raila Odinga, na kukosekana kwa uhakika wa iwapo Rais Kenyatta na wafuasi wake watamuunga mkono naibu wake kuwania urais mwaka 2022.

Joto linaripotiwa kuwa jingi ndani ya chama hicho kutokana na tofauti kati ya mrengo wa kilichokuwa chama cha TNA kilichoongozwa na Rais Kenyatta dhidi ya URP kilichosimamiwa na William Ruto. Vyama hivyo vilivunjwa mwaka 2017 na kuungana kubuni Jubilee.

Katika kile kinachobainika kuwa kujiandaa kwa talaka inayoweza kutokea ndani ya Jubilee wakati wowote, baadhi ya wabunge washirika wa Naibu Rais wameunda vyama vya kisiasa na kutangaza wazi kwamba wanamwandalia kinara wao chama cha kuingia ikulu, iwapo wandani wa Rais Kenyatta “wamsaliti” na kukosa kusimama naye 2022.

Wadadisi wanasema japo Bw Ruto ameepuka kuzungumzia suala hilo hadharani, washirika wake wa kisiasa wamechukua hatua zinazoweza kuvunja chama cha Jubilee, alichotarajiwa kutumia kugombea urais 2022.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei amenukuliwa akisema wanalenga kutayarisha chama ambacho Bw Ruto atatumia kugombea urais 2022. “Kama marafiki wa William Ruto, tunapanga kuunda chama chetu. Tunafikiria kumwachia Rais Uhuru na watu wake chama cha Jubilee,” alisema Bw Cherargei.

Naye mwandani wa Bw Ruto, ambaye aliomba asitajwe alisema: “Subiri tu, tunaandaa mikakati, ndoa yetu na upande wa Rais Kenyatta katika Jubilee inayumba, na sio siri.”

Hatua ya Rais Kenyatta kuingia kwenye mwafaka na Bw Odinga mapema mwaka huu nako kumeonekana kuongeza kasi ya mtafaruku katika Jubilee, baada ya mrengo wa Naibu Rais kutafsiri hatua hiyo kama mbinu ya kuhujumu ndoto yake ya kuwa rais.

Vita dhidi ya ufisadi viliposhika kasi, washirika wa kisiasa wa Bw Ruto walianza kulia ngoa wakidai vinaendeshwa kwa ubaguzi.

Msukosuko huo ulizorota baada ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa watumishi wote wa umma wafafanue walivyopata mali yao katika juhudi za kupigana na ufisadi.

Bw Cherargei, Mbunge Oscar Sudi na kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen walijitokeza na kupinga agizo hilo wakidai lilimlenga Bw Ruto.

Siku tatu baada ya Bw Murkomen kujitokeza kimasomaso kudai Bw Ruto ndiye mlengwa wa tangazo kuhusu ufafanuzi wa mali, iliibuka kuwa wandani wa Bw Ruto wamesajili vyama vipya vya kisiasa vya United Green Party (UGP) na Grand Dream Development Party (GDDP).

Mgawanyiko wa Jubilee umepenya hadi bungeni. Mnamo Jumanne, Mbunge wa Aldai, Cornelly Serem alidai kuwwa nduguye Rais Kenyatta, Muhoho Kenyatta ni mmoja wa walioagiza sukari mbaya, jambo ambalo Wizara ya Kilimo imekanusha ikisema jina lake liliingizwa na watu wenye nia mbaya kwenye orodha iliyowasilishwa.

Hapo jana, Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, alimtaka Murkomen na mwenzake katika bunge Aden Duale kujiuzulu kwa kile alichosema ni kuvuruga vita dhidi ya ufisadi.

Bw Wambugu aliwalaumu Duale na Murkomen kwa madai ya kuhujumu juhudi za Rais Kenyatta kupigana na uovu huo akidai wanawatetea baadhi ya wanaolaumiwa kwa kuingiza sukari yenye sumu nchini, na kupinga wanasiasa na watumishi wa serikali walivyopata mali yao.

“Hatuwezi kuwa na viongozi wa wengi wanaotumiwa kumshambulia Rais. Walipatiwa nyadhifa hizo kutetea sera za Rais na sio kuzipinga. Wanafaa kujiuzulu au tuwatimue,” alisema Bw Wambugu.

Mbunge huyo, ambaye mapema mwaka huu alizua mjadala kwa kudai si lazima wafuasi wa Rais Kenyatta wamchague Bw Ruto 2022, alitisha kuwarai wabunge na maseneta wengine wa Jubilee kuwatimua wawili hao kutoka nyadhifa zao na kuteua watu wengine.

Alisema hatua ya Bw Serem, ambaye ni mwandani wa Ruto ya kutaja jina la Bw Muhoho kwenye kikao cha kamati ya bunge mnamo Jumanne, ilikuwa ni njama ya kumtisha Rais Kenyatta ili aache vita dhidi ya ufisadi.

Bw Wambugu alidai baadhi ya wabunge wenzake wanawalenga jamaa za familia ya rais ili kuhujumu vita dhidi ya ufisadi na biashara ya magendo ili kulinda baadhi ya kampuni.

Naye Bw Duale, ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto, amekuwa akikosoa juhudi za kusaka sukari ya magendo zinazoendelezwa na serikali.

Bw Wambugu alisisitiza kuwa viongozi hao wawili wanafaa kuunga mkono ajenda za Rais badala ya kuzipinga akisema hawafai kushikilia nyadhifa za viongozi wa wengi.