Jubilee yawaonya vikali madiwani wa ngome ya Ruto wasiopigia debe BBI

Jubilee yawaonya vikali madiwani wa ngome ya Ruto wasiopigia debe BBI

Na ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha Jubilee sasa kimewaonya vikali madiwani walioteuliwa kutoka ngome ya kisiasa ya Naibu Rais, William Ruto, Kaskazini mwa Bonde la Ufa, dhidi ya kulemaza Mswada wa kurekebisha Katiba kupitia BBI.

Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Raphael Tuju aliwaeleza madiwani kwamba, huenda wakaadhibiwa endapo watapiga kura kupinga BBI huku chama hicho kikianzisha mikakati kabambe ya kuwashawishi madiwani zaidi kuunga mchakato huo.

Tuju alikutana na madiwani maalumu kutoka Uasin Gishu kwenye kikao kilichoandaliwa katika makao makuu ya chama hicho Pangani, Nairobi.Katika barua fupi walioandikiwa, madiwani walialikwa kuhudhuria mkutano huo ambao ajenda yake ilijitokeza kuwa uungwaji mkono wa BBI.

Duru zasema kwamba, katika mkutano huo uliohudhuriwa na madiwani wote 17 maalumu, Bw Tuju aliwaelekeza kupiga kura kuiunga mkono BBI la sivyo wapoteze nyadhifa zao.

“Tuju alitueleza kuwa ni sharti tufuate msimamo wa chama kuhusu BBI la sivyo tutachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisema Bw Edwin Misoi, mmoja wa madiwani hao.

Bw Misoi alisema ingawa chama kinawataka kupitisha BBI, mswada huo utaidhinishwa au kukataliwa kwa kutegemea uamuzi wa wakazi.

“Tunaunga mkono ushirikishaji wa umma. Maoni tutakayopata kutoka kwa wananchi ndiyo tutakayofuata,” alisema.

Mswada wa BBI uliwasilishwa katika Bunge la Kaunti hiyo wiki iliyopita na umekuwa ukijadiliwa na umma kabla ya madiwani kuujadili na kupiga kura.

Mkutano sawa na huo uliofanyika wiki jana kati ya Bw Tuju na madiwani wa Baringo ulisababisha hofu baada ya madiwani maalumu kudaiwa kushurutishwa kupiga kura kuunga mkono BBI au wapoteze viti vyao, jambo walilolipiza kisasi baadaye kwa kutupilia mbali BBI.

Mabunge ya Kaunti za Pokot Magharibi na Trans Nzoia zilikuwa za kwanza kupitisha Mswada wa marekebisho ya kikatiba eneo la Bonde la Ufa, ambalo ni nyumbani kwake Dkt Ruto.

You can share this post!

Kila familia kulipa Sh6,000 katika mageuzi mapya NHIF

Elachi atunukiwa Unaibu Waziri Uhuru akipanua serikali yake