Michezo

Jude Bellingham aitwa kuunga kikosi cha Uingereza kwa mara ya kwanza

November 11th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

TINEJA Jude Bellingham, 17, amejumuishwa katika timu ya taifa ya watu wazima ya Uingereza kwa mara ya kwanza.

Kiungo huyo wa Borussia Dortmund amekwezwa ngazi kutoka kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 baada ya beki Trent Alexander-Arnold wa Liverpool na kiungo James Ward-Prowse wa Southampton kuondolewa na kocha Gareth Southgate kwenye timu yake kwa sababu ya majeraha.

Bellingham aliingia katika sajili rasmi ya Dortmund mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana na Birmingham ya Uingereza. Tangu wakati huo, amewajibishwa na waajiri wake wapya mara 11.

Uingereza wamepangiwa kuchuana na Jamhuri ya Ireland, Ubelgiji na Iceland kati ya Novemba 12 na 18, 2020.

Iwapo Bellingham atachezeshwa katika mechi yoyote kati ya hizo, basi atakuwa mwanasoka wa tatu mwenye umri mdogo zaidi baada ya Theo Walcott na Wayne Rooney kuwahi kuwakilisha Uingereza.

Bellingham aliwajibishwa na Birmingham kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 2019 na akavalia jezi za kikosi hicho mara 44 kabla ya kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Dortmund baada ya kushawishiwa kwa Sh4.2 bilioni.

Bellingham aliitwa kambini mwa Uingereza U-21 kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 2020 na akaweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibikia kikosi hicho alipochezeshwa dhidi ya Kosovo mnamo Septemba 4, 2020.

Mvamizi Marcus Rashford wa Manchester United atakosa mechi ya Uingereza dhidi ya Jamhuri ya Ireland kwa kuwa anatarajiwa kuungana na wenzake kikosi mnamo Novemba 12 baada ya kupata jeraha alipokuwa akicheza dhidi ya Everton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 7 ugani Goodison Park. Man-United walisajili ushindi wa 3-1 katika mechi hiyo baada ya kufungiwa mabao na Bruno Fernandes na sajili mpya Edinson Cavani.

Baada ya Bellingham kukwezwa ngazi hadi timu ya watu wazima kambini mwa Uingereza, kocha wa Uingereza U-21, Aidy Boothroyd amewaita makinda wawili wa Everton –  Tom Davies na Ben Godfrey kujaza pengo hilo na lile la Max Aarons wa Norwich City ambaye atakosa mechi zijazo dhidi ya Andorra na Albania mnamo 13 na 17 kutokana na jeraha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO