Makala

JUHUDI: Mkulima asema kukiwa na utaratibu mzuri, ni rahisi kujenga mabwawa

June 15th, 2019 2 min read

NA SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Jubilee ilipochukua hatamu 2013 chini ya kinara Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt Willima Ruto, iliingia kwa kishindo na ahadi chungu nzima kwa Wakenya.

Kuanzia ujenzi wa barabara, uimarishaji elimu, afya, kilimo, ni miongoni mwa ajenda ilizoahidi Jubilee kwenye manifesto yake.

Mwaka 2017 Rais Kenyatta alizindua mpango aliosema anataka Wakenya wamkumbuke kwa angalau mambo manne ambayo ni makao ya bei nafuu, kuwepo kwa chakula cha kutosha, matibabu bora kwa wote na kwa bei nafuu pamoja na uundaji wa viwanda.

Ili kuafikia ajenda ya kuwepo kwa chakula cha kutosha, serikali imekuwa ikizindua miradi ya uchimbaji wa mabwawa katika sehemu mbalimbali nchini ili kuimarisha sekta ya kilimo.

Ni miradi ambayo imepangiwa mabilioni ya pesa, na kufikia sasa nyingi yayo ingali kitendawili. Isitoshe, imekumbwa na ubadhirifu wa fedha ilizotengewa na Wizara ya Fedha.

Serikali inaendelea kukosolewa kwa miradi iliyogeuka kuwa hewa ilhali imetengewa mgao wa kuifanikisha.

Kilomita chache kutoka mji wa Naromoru, Kieni kaunti ya Nyeri, mkulima mmoja ni kielelezo kwa serikali katika uchimbaji wa bwawa.

Serikali ikitumia mabilioni ya pesa kufanikisha hilo, Timothy Mburu ana bwawa lililomgharimu kiasi chini ya Sh1.5 milioni.

Ni shughuli aliyoifanya kati ya 2011-2012, kabla ya kuvalia njuga suala la ukulima.

“Ilinigharimu Sh1.2 milioni kulichimba na kufikia sasa limekuwa lenye manufaa chungu nzima kwangu,” anasema Bw Mburu.

Anasema ni kazi aliyofanya mara baada ya kupata idhini kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Utunzaji Mazingira (Nema).

Bwawa hilo lililoko katika kijiji cha Gitinga, lina uwezo wa kusitiri zaidi ya lita milioni 40 ya maji.

Ameliundia mtaro ulio karibu futi mbili kuenda chini na urefu wa mita mia tano unaoteka maji msimu wa mvua na kuyaelekeza kwenye bwawa.

“Mvua inaponyea huhakisha matone ya maji hayapotei. Haijalishi ni mvua kiasi gani, hata ile ya rasharasha inayopita kufukuza wavivu shambani,” anaeleza.

Meshack Wachira, mtaalamu wa masuala ya kilimo anasema malalamishi ya njaa Kenya wakati wa kiangazi yanaweza kuwa historia endapo serikali itaiga mkondo wa Bw Timothy Mburu.

Tana River, Narok, Turkana, Baringo, Kitui, Marsabit, Samburu, Garissa, Mandera na Wajir, ni baadhi ya kaunti zinazoshuhudia ukame.

Kaunti zingine ni Pokot Magharibi, Kilifi, Isiolo, Laikipia, Taita Taveta, Makueni, Kajiado na Lamu.

“Hizo ni kaunti ambazo mafuriko yanapotokea hazikosi kuathirika. Yakichimbiwa mabwawa sawa na la Bw Mburu, maji hayo yatavunwa na kutumika kufanya kilimo msimu wa kiangazi. Kwa gharama aliyounda lake, nchi hii itakuwa na mabwawa mengi sana,” anashauri Bw Wachira.

Kenya, mvua kubwa huwa kati ya Machi hadi Juni. Miezi mingine kuna baadhi ya maeneo ambayo pia hupata mvua, ingawa kiasi.

Nchi kama Misri na Israili ni kame, na mengi ya matunda kama vile; matufaha na zabibu hutoka huko.

“Eneo la Naromoru pia huwa kame. Tukiiga mkondo wa mataifa kama hayo Kenya itakuwa na chakula cha kutosha,” asema Bw Mburu.

Wakulima wengi humo hutegemea maji ya mvua, baadhi yao wakijaribu kufuata mkondo wa Mburu kuvuna maji.

Naromoru ni miongoni mwa maeneo yanalozalisha viazimbatata kwa wingi.

Pia, ni tajika katika kilimo cha vitunguu na kabichi. Vilevile, hukuza mahindi yanayokua kwa kipindi kifupi.