Makala

JUHUDI NA MALENGO: Alichoka na vibarua akaona ageukie mboga na matunda

June 13th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KAUNTI ya Kirinyaga ni miongoni mwa maeneo ya humu nchini ambayo yanaongoza katika kilimo cha nyanya.

Kikubwa kinachowezesha eneo hili kuwa mstari wa mbele katika kilimo cha mimea hii ni hali nzuri ya hewa yenye joto na baridi ya wastani katika baadhi ya sehemu.

Zaidi ya hayo, wakulima wengi wamewekeza katika masuala ya unyunyiziaji maji kwa mimea.

Vijana wengi nchini husema ya kuwa hamna kazi kwa vile kazi wanazozitafuta mara nyingi ni za ofisini baada ya kuhitimisha masomo ya viwango mbalimbali.

Hali hii ni tofauti kabisa kwa James Waweru mwenye umri wa miaka 29.

Huu ni mwaka wake wa sita sasa akijishughulisha na kilimo cha nyanya, maharagwe, matunda na mboga mbalimbali za kiasili.

Mawazo haya yalimjia baada ya kukamilisha safari yake ya elimu katika shule ya upili na kufanya vibarua vya kila sampuli bila ya kuona lolote kubwa la kujivunia wala kuonea fahari.

Anaelezea kuwa kilimo cha nyanya kinahitaji uekezaji mkubwa wa kiwango na hali ya juu na vilevile muda mwingi kutoka kwa mkulima mwenyewe.

Kwa kawaida huwa anahitajika kunyunyizia mimea yake maji mara mbili kwa wiki ili kuiwezesha kukua kwa haraka na kwa afya bora.

Maji haya huwa anayatoa hatua chache kutoka kwa mkondo wa maji uliopitia karibu na shamba lake ambako huwa anatumia mashine ya kueneza maji hadi shambani.

Kulingana naye, nyanya huhitaji muda wa hadi siku 60 (miezi miwili) ili zianze kumpa mkulima mavuno yaafayo. Katika sehemu ya shamba lake la ekari moja na robo, huwa ananunua mbegu na kuzipanda kwenye kitalu kwanza.

Nyanya zinapokua, huwa anatia mbolea za madukani pamoja na zile za kiasili ili kuupa mchanga madini muhimu inavyohitajika.

Mimea inapozidi kukua na nyanya kuwa nzito kiasi cha kuanza kulemea mashina ya mimea yenyewe, huwa anaiwekea vijiti ili kuipa matawi msaada wa kujishikilia.

Hatua hii pia huzuia nyanya kugusa chini mchangani na hivyo kuepukana na uharibifu, hasa hali ya kuoza.

“Katika shamba la ekari moja, huwa napanda miche zaidi ya elfu saba na baada ya miezi mitatu, nyanya huwa zimeanza kukomaa ambapo huwa naanza kuvuna mara mbili kwa wiki. Shughuli hii ya kuvuna huwa naifanya kwa miezi miwili kabla ya nyanya kuisha kabisa shambani,” Bw Waweru anasema.

Uuzaji

Katika kila sanduku la nyanya, kwa kawaida huwa anauza kati ya Sh2,500 na Sh3,000 kulingana na msimu na mavuno yanayopelekwa sokoni na wakulima wengine.

Mapato anayopata kutokana na mauzo ya bidhaa hii yamemwezesha kununua kipande kingine cha shamba na kujengea familia yake makao.

Pia, ameweza kununua ng’ombe wa maziwa ambao anawalisha nyumbani na katika shamba lake kila baada ya msimu wa mavuno.

Baadhi ya changamoto ambazo anapitia katika ukulima wake ni pamoja na upungufu wa maji katika misimu ya jua kali na vilevile ushindani mkubwa wa bei ambako bei hushuka wakati kuna mavuno mengi ya bidhaa hii katika sehemu nyinyinezo za chini.

Changamoto nyingine bei ya mafuta ya petroli anayohitaji kwenye pampu ya maji.