Makala

JUHUDI NA MALENGO: Kundi laanza biashara pevu ya uyoga kupitia ufadhili wa Kaunti

June 13th, 2019 2 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

KUNDI la vijana la Maweni Youth Initiative Group mjini Taveta lenye makao katika eneo la Kambini, Bura Ndogo, limebuni mbinu ya uwekezaji wa kisasa kufikia ruwaza ya 2030 ya miradi ya maendeleo kwa vijana.

Akilimali imegundua mikakati ya mradi wa kipekee wa ukuzaji uyoga unaoendeshwa na kundi hili lenye wanachama wapatao 18.

Akihojiwa kwenye eneo la mradi huu, mwenyekiti wa kundi hili Juma Tutu Makau anasema kabla ya kujitosa kwenye shughuli ya ukuzaji uyoga, kundi hili lilianza ufugaji wa takriban kuku 150 kabla ya kufadhiliwa na serikali ya kaunti ya Taita Taveta.

‘Tulianzisha mradi wa ufugaji kuku uliodhaminiwa na serikali ya kaunti, iliyoona juhudi zetu na kutuahidi hundi ya Sh500,000 mnamo Januari 19, 2018,” anadokeza Juma Tutu Makau.

Mwenyekiti huyo anasema baada ya kuahidiwa hundi hiyo, kamati ilikabidhiwa rasmi Aprili mwaka huu, na mikakati ikafanywa kuanzisha mradi mpya wa ukuzaji uyoga.

‘Tuliamua kuanzisha ukuzaji uyoga sawa na kuagiza kuku wengine 100 zaidi huku Serikali ya Kaunti ikiahidi kutupatia kuku wengine 100 zaidi kama hatua ya kuboresha utendakazi wetu kwenye mradi huu,” anafichua Makau.

Kuhusu shughuli za ukuzaji uyoga, mwenyekiti huyo anadokeza kuwa kundi lake tayari limepanga kuwa na mabanda 6 makubwa ya ukuzaji wa zao hilo.

“Tuna mpango wa kuwa na mabanda 6 ambayo kila moja litakuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 300 za uyoga,” aarifu.

Mwenyekiti huyo anasema kuwa kilo moja ya uyoga inauzwa kwa Sh400 kwenye masoko ya kijamii mbali na kwamba kawaida huuzwa kwa Sh800.

Juma anasema Oyster ni aina ya uyoga inayokuzwa na kundi hili, na kwamba ina manufaa mengi yakiwemo kutibu shinikizo la damu mwilini mbali na kuwa chakula bora kwa afya ya mwanadamu na pia mbolea kwa wakulima inapouzwa ikiwa ingali mbichi.

Makau anakiri kuwa soko kuu la zao la uyoga ni hotelini.

‘Tungu tuanze kukuza uyoga, soko letu kubwa ni kwenye hoteli za kitalii kama vile Sarova (Taita), Lima (Eldoret) na Naivas (Mombasa)’ aelezea huku akidai kundi lake hutia saini mkataba kati yao na wateja wa miezi kumi kuhusiana na mauzo ya bidhaa hiyo.

“Tunafanya hivyo ili kujenga uhusiano mwema wa kibiashara sawa na uaminifu kati yetu na wateja,” asema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, imebainika kuwa shughuli za mradi wa ukuzaji uyoga ni ngumu mno kwa wakulima wachanga.

“Tunakatakata mabaki ya ngano na kuyaloweka majini kabla ya kuyachanganya na vimelea vya mbegu za pamba pamoja na chokaa, kisha tunazitumia kama mchanga wa kukuzia uyoga,” anadokeza Makau.

Mabaki ya ngano

Aidha, anasema kuwa kundi lake huagiza mabaki ya ngano, vimelea maalumu vya pamba pamoja na chokaa kutoka Nairobi.

“Tunazingatia mno usafi kwenye shughuli hii. Kabla ya kuanza shughuli yenyewe ni lazima tujipige au kujinyunyizia spirit mwili mzima. Baada ya kufanya hivyo tunatia lita 60 za maji ndani ya pipa lenye kichujio katikati halafu tunatandaza majani juu yake na kuyachemsha kwa muda wa saa sita kabla ya kuyapakua,” anapasha Akilimali.

Mwenyekiti huyo asema kuwa kundi lake huagiza mbegu za zao la uyoga kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta kilichoko jijini Nairobi.

Anasema mpango mzima wa uzalishaji uyoga huchukua siku 7 ndani ya Curator kabla ya mbegu kuhamishwa rasmi kwingineko kwa ukuzaji, kwa siku zingine 28.

“Baada ya hapo tunasubiri kwa kati ya siku hizo 28 hadi 38 kwa mavuno kamili,” anasema Juma Tutu Makau.

Kundi la Maweni Youth Initiative ndilo kundi la pekee mjini Taveta ambalo linatambuliwa rasmi na serikali ya Taita Taveta kwa shughuli za mradi huo wa ukuzaji uyoga.

Ni kundi ambalo tayari limeona faida ya ukuzaji uyoga, na sasa linataka kujipanua zaidi kufikia ruwaza ya maendeleo ya vijana ya 2030.