Habari Mseto

Juhudi za kuimarisha chakula cha kutosha nchini zaongezeka

October 24th, 2018 2 min read

RICHARD MAOSI NA MAGDALENE WANJA

MIONGO mitatu iliyopita Kenya imeshuhudia kupungua kwa kiwango cha chakula zaidi ya asilimia 10, ndipo mikakati kabambe ikabuniwa kuangazia tatizo hili.

Suala lenyewe limefanya taifa kuagiza chakula kutoka mataifa ya nje licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kijitosheleza.

Kutokana na mradi wa Zero Hunger Strategy Review,uzalishaji mahindi ni chini ya tani 2 katika kila hekta 100 ,ingawa inaweza kuzalisha tani 6.

Wananchi wengi wanategemea mahindi,viazi tamu,mchele na ngano kama lishe pendwa ya mara kwa mara inayoshabikiwa na watumiaji wengi.

“Kenya ni taifa ambalo linaongoza Afrika Mashariki katika uagizaji wa chakula hasa ngano na mchele kutoka nje yapata bilioni 130 kila mwaka,”ripoti inaeleza.

Vilevile inaaminika kwamba kuongezeka kwa idadi ya watu,ndio chanzo cha kutatiza uwezo wa kulisha watu.

Katika kongamano la kuzindua mradi wa Zero Hunger Strategy Review siku ya chakula duniani,iliyofanyika kaunti ya Nakuru Katibu mkuu wa Huduma za lishe katika wizara ya kilimo,daktari Andrew Tuimur alisema asilimia 25 ya uvumbuzi katika sekta ya kilimo barani Afika zilianzishwa Kenya.

Afisa wa kilimo kutoka Kaunti ya Naivasha wakionyesha namna uvumbuzi wa kisasa unaelekea kufaa uzalishaji kidijitali. Picha/ Richard Maosi

“Hii ni ishara tosha kwamba Kenya inamudu kujitosheleza kukabili changamoto za chakula,”alisema.

Kulingana na ripoti kuna mambo kadhaa yaliyochangia uzalishaji wa chakula duni.

Ni pamoja na kutegemea mvua,kutojiandaa mapema msimu wa kupanda na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ha hali ya anga.

“Unyunyizaji ni mgumu kutekeleza kwa sababu vyanzo vya maji havipatikani katika kila sehemu ya nchi,wakulima wadogo ndio hutaabika Zaidi,”alisema.

Kulingana na ramani ya ‘National Water Master Plan’ 2030 kina cha ukulima kimefikia hekta milioni 2.9 ambapo ni asilimia 4 hupata huduma za kunyunyiza mashamba.

Kiangazi na masika kila msimu ni njia nyingine ya kubainisha kwamba bado taifa halijajiandaa katika hatua za kukabiliana na matatizo yanayowakumba wakulima.

Kaunti 8 ziliangaziwa kwa kuadhirika na kiangazi kati ya 2011 na 2016.Miongoni mwao ni Turkana,Marsabit,Samburu,Isiolo,Wajir,Taita Taveta na Kajiado.

Mambo mengine yanayochangia ukosefu wa ubora katika mazao ni pamoja na Uharibifu wa mazingira,ukosefu wa rutuba mchangani na kutotumia masine shambani kuongeza mazao.

Kenya inatarajia kutimiza ruwaza ya 2030 ambapo azma ya kupata chakula cha kutosha ni miongoni mwa ajenda zake kuu.