Habari Mseto

Juhudi za kukabiliana na Al-Shabaab msituni Boni ziongezwe – Viongozi wa Lamu

April 2nd, 2018 2 min read

Mbunge wa Lamu Mashariki, Sharif Athman akiohijwa na Taifa Leo. Picha/ Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI wa kaunti ya Lamu wanaitaka serikali ya kitaifa kuongeza jitihada zaidi katika makabiliano dhidi ya Al-Shabaab kwenye msitu wa Boni.

Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud na Mbunge wa Lamu Mashariki, Athman Sharif, wameeleza haja ya serikali kutia makali vita dhidi ya Al-Shabaab ili kurejesha amani na utulivu katika Wadi ya Basuba na sehemu zote za mpakani mwa Lamu na Somalia.

Wakizungumza na wanahabari Jumapili, viongozi hao walikiri kuwa masuala mengi ya kimsingi, ikiwemo elimu hayajakuwa yakitekelezwa ipasavyo hasa kwenye eneo la Basuba kufuatia hali duni ya usalama inayochangiwa na Al-Shabaab.

Bw Aboud alisema shule zote tano za Basuba, ambazo ni Milimani, Mangai, Mararani, Kiangwe na Basuba hajizaweza kuendeleza masomo muhula wote kama inavyofanyika sehemu nyingine za nchi kufuatia ukosefu wa walimu na taharuki ya kila siku inayochangiwa na Al-Shabaab.

Alisema masomo yanayoendelea kwenye shule hizo kwa sasa ni yale ya chekechea (ECDE) pekee ilhali kaunti ikilazimika kuwahamisha baadhi ya wanafunzi hadi Kiunga na Mokowe ili kuendeleza masomo yao.

Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud. Picha/ Kalume Kazungu

“Tunaloomba ni serikali kuzidisha nguvu makabiliano dhidi ya Al-Shabaab kwenye msitu wa Boni. Magaidi hao wamepelekea masomo kusambaratika eneo la Basuba.

Walimu hawataki kupelekwa kuhudumia eneo la Basuba na hiyo ni changamoto kubwa. Shule nyingi eneo hilo bado hazijafunguliwa ilhali wanafunzi wa ECDE pekee ndiop wanaendelea na masomo. Usalama ukiimarishwa, maisha ya wakazi wa Basuba pia yatarejelewa kama kawaida,” akasema Bw Aboud.

Naye Bw Sharif alieleza haja ya ushirikiano kati ya wadau wote ili kufanikisha vita dhidi ya Al-Shabaab hapa nchini.

Alisema anaamini ushirikiano uliopo kati ya serikali ya kitaifa na viongozi wa kaunti utasaidia kumaliza vita dhidi ya Al-Shabaab kote Lamu.

Bw Sharif alisema tayari wamefanya mazungumzo na idara ya usalama katika kuhakikisha usalama unadhibitiwa Basuba na Lamu kwa jumla.

“Tuzidi kushirikiana ili kuiwezesha serikali kuu kufaulisha vita dhidi ya Al-Shabaab. Ninaamini ugaidi ukimalizwa eneo hili, masomo na shughuli nyingine za maisha zitarejelewa kama kawaida,” akasema Bw Sharif.

Shule tano za Basuba zilifungwa tangu 2015 baada ya walimu waliokuwa wakihudumu eneo hilo kutoroka vitisho vya Al-Shabaab.

Aidha mapema mwaka huu, serikali kuu ilikuwa imeagiza kufunguliwa kwa shule zote za Basuba, japo kufikia sasa hatua hiyo haijatekelezwa kutokana na ukosefu wa walimu na miundomsingi duni ya elimu eneo hilo.