Habari za Kitaifa

Juhudi za mwanamke kusimamisha mazishi ya Kiptum zagonga mwamba

February 22nd, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

JUHUDI za mwanamke wa umri wa miaka 22 kupinga mazishi ya mwanariadha Kelvin Kiptum ziligonga mwamba baada ya mahakama kuu mjini Eldoret kukataa kutoa agizo la kusitisha mazishi hayo.

Mwanamke huyo andai kuzaa mtoto msichana na marehemu na kwamba hajatambuliwa na familia ya marehemu kama mmoja wa warithi wake.

Katika ombi lake mbele ya jaji Robert Wananda, Edna Awuor Otieno alitaka mahakama isitishe maziko hadi atambuliwe pamoja na mtoto wake kama warithi wa mali ya mwendazake.

Kupitia kwa ombi la dharura, Edna alifika kortini kuzuia mwili wa marehemu kuondolewa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Eldoret kwa maziko kabla ya kusikizwa kwa ombi lake.

Katika ombi lake kupitia kwa wakili Joseph Oyaro, pia aliomba mahakama itoe amri ya kuchukua sampuli za DNA kutoka kwa mwili wa marehemu ili zipelekwe katika Taasisi ya Utafiti wa Kiafya ya Kenya au taasisi nyingine yoyote ya umma kwa madhumuni ya kuthibitisha asili ya baba ya mtoto husika.

Aliiambia mahakama mtoto huyo ni binti wa kumzaa wa marehemu na hivyo ana haki ya kunufaika na mali ya mamilioni ya pesa iliyoachwa na marehemu.

Alimweleza Jaji kwamba familia ya marehemu haikukataa tu kumtambua kama sehemu ya familia na pia ilikosa kujumuisha jina la mtoto wake kwenye orodha ya watoto walioachwa kama inavyotarajiwa.

Mlalamishi alisema kuwa kabla ya kifo cha Kiptum kupitia ajali ya barabarani marehemu alikuwa akimhudumia mtoto mchanga na vile vile kutunza mahitaji yote ya mtoto.

“Marehemu alikuwa amenitambua mimi na mtoto wake na amekuwa akitutunza vizuri kama sehemu ya familia yake hadi kifo chake wiki mbili zilizopita,” alisema mlalamishi.

Aidha, alifichua kuwa siku ya ajali Kiptum aliwasiliana naye akitaka kujua jinsi mtoto huyo anavyoendelea na kuahidi kumtumia pesa za kumtunza na mahitaji mengine ya kimsingi.

Huku akikataa ombi hilo, Jaji Wananda alisema kwamba mazishi ya marehemu Kiptum yalikuwa ya manufaa kwa umma hivyo hangetoa agizo la kuzuia mazishi hayo.

“Mipango ya mazishi ya marehemu iko katika hatua za mwishomwisho na hivyo basi kusimamisha maziko kunaweza kuleta usumbufu kwa kuzingatia rasilimali zilizowekwa katika maandalizi ya mazishi,” aliamua Jaji Wananda.

Kuhusu suala la mtoto kupata haki ya malezi bora alisema kuna njia nyingine za kisheria ambazo mama huyo na uhuru wa kuzitumia kutafuta kuthibitisha baba wa mtoto huyo.

“Kwa hivyo masilahi ya mtoto mchanga hayatapuuzwa kwa amri hii, kwa hivyo mama wa mtoto yuko huru kutumia njia zingine za kisheria ili kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinatunzwa vizuri,” alisema hakimu.

Wakili anayemwakilisha hakupinga agizo la mahakama bali alikubali kuwa atatafuta njia nyingine ya kisheria kuhusu suala hilo hata baada ya mazishi.