JUKWAA WAZI: Murkomen ‘amkaribisha’ rasmi Natembeya siasani kwa mishale mikali

JUKWAA WAZI: Murkomen ‘amkaribisha’ rasmi Natembeya siasani kwa mishale mikali

Na WANDERI KAMAU

BAADA ya kutangaza kujitosa kwenye ulingo wa siasa mapema mwezi huu wa Januari, aliyekuwa Mshirikishi Mkuu wa eneo la Bonde la Ufa, Bw George Natembeya ameanza kujipata kwenye majibizano na wanasiasa.

Bw Natembeya ametangaza atawania ugavana katika Kaunti ya Trans-Nzoia kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Bw Natembeya tayari ameanza kampeni zake, akitaja ufanisi mkubwa aliopata akiwa mshirikishi mkuu kama hali inayoashiria ndiye chaguo bora zaidi kwa wenyeji wa Trans Nzoia.

Hata hivyo, kauli yake ilipingwa vikali na Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), akisema hakuna ufanisi wowote aliopata, bali alikuwa akitumia vyombo vya habari kujitangaza.

Tayari, imeibuka huenda afisa huyo wa zamani akawania nafasi hiyo kupitia chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K), kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa.

George Natembeya (anayelenga kuwania ugavana Trans Nzoia): “Niliipenda sana kazi yangu. Niliipenda sare niliyovalia. Mimi ni miongoni mwa washirikishi ambao walitumia muda wao mwingi wakiwahudumia wananchi. Ikiwa ningeendelea kuhudumu katika nafasi hiyo, ni wazi kuwa serikali mpya ingenipandisha ngazi kuwa Katibu wa Wizara au Waziri. Wenyeji wa Trans Nzoia watakuwa na bahati sana kuwa nami kama gavana wao.

Kipchumba Murkomen (Seneta, Elgeyo Marakwet): “Ninasikia George (Natembeya) anafanya kampeni akieleza mafanikio aliyopata alipohudumu kama Mshirikishi Mkuu wa eneo la Bonde la Ufa. Anasema ndiye mshirikishi pekee aliyefaulu kuboresha usalama katika eneo hilo. Ni kama marehemu Yusuf Haji na Ishmael Chelang’a hawakuhudumu kama wakuu wa mkoa huo katika miaka ya ’90. Hakuna ufanisi wowote alipata kwa miaka miwili aliyohudumu.”

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: PAA yayumba kuhusu itakayeunga kwa urais

Raila na Ruto wararuana vikali Mlimani

T L