NA WANDERI KAMAU
KULIPA ushuru ni kujitegemea. Ndiyo kauli ya Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA).
Hata hivyo, swali linaloibuka ni: Wakenya wote kweli wamekuwa wakilipa ushuru kama inavyohitajika kisheria?
Uongozi wa Kenya Kwanza unamlaumu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya kuweka mikakati ya kuhakikisha biashara zinazomilikiwa na familia yake hazilipi ushuru.
Ndio ujumbe uliotolewa na maseneta kadhaa kutoka mrengo huo, wakiongozwa na Seneta John Methu (Nyandarua).
Maseneta hao wanadai kuwa na ripoti za kijasusi zinazoonyesha kampuni za familia ya Bw Kenyatta zimekuwa zikikwepa kulipa ushuru.
Hata hivyo, Bw Kenyatta alipuuzilia mbali madai hayo, akiyataja kuwa “kelele” za watu walioshindwa kufanya kazi. Swali ni: Ni nani msema kweli?
John Methu-Seneta, Nyandarua
“Kama Maseneta, tuna ripoti za kijasusi kuhusu wale wanaofadhili mikutano ya kisiasa ya mrengo wa Azimio baada ya kushinikizwa kulipa ushuru. Tungetaka kuwarai Wakenya kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwa manufaa yao wenyewe ili kujikinga dhidi ya kutoulizwa maswali yanayohusu ulipaji ushuru. Tutairai KRA kuchunguza kiasi cha ushuru ambao familia ya Kenyatta haijalipa kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita.”
Uhuru Kenyatta-Rais Mstaafu
“Msihofishwe na watu hawa wanaopiga kelele. Watu ambao hawana lolote la kufanya daima watapiga kelele. Hayo ni maisha. Sisi tutaendelea na shughuli zetu kama kawaida.”
Subscribe our newsletter to stay updated