Bambika

Juliani aapa kunyanyuka tena baada ya jengo lake kubomolewa

June 7th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

RAPA Julius Owino almaarufu Juliani, amejipa imani kwamba kwa uwezo wa Mungu, atanunua majengo zaidi jijini Nairobi baada ya kituo chake cha Hip Hop City, Dandora, kubomolewa na serikali.

Kituo hicho ambacho kilianzishwa miaka saba iliyopita, mwazilishi akiwa na nia ya kulea vipaji vya vijana kutoka Dandora, kilibomolewa kufuatia agizo la serikali kutokana na kuwa ndani ya mita 30 kutoka kwenye mto.

Katika mahojiano, mwanamuziki huyo alisema ubomoaji huo haukumbabaisha kivyovyote vile, akieleza tu kuwa jengo hilo alipewa na Mungu na yeye ni msimamizi tu.

“Huwezi kuelewa kazi ya Mungu. Ninaendelea kuwaambia watu kwamba kila kitu ambacho nimewahi kukijenga, kwa kawaida nakiona kuwa ni cha Mungu na mimi ni msimamizi tu. Anaweza kukirudisha wakati wowote. Si changu… ni mali ya Mungu,” alisema Juliana.

Juliana aliongeza kuwa hakuona haja ya kupinga ubomoaji huo.

Alisistiza Mungu ndiye aliyempa rasilimali za kununua jengo hilo na vitu vingine.

“Wenyeji walitaka kufanya maandamano na pengine kumchunguza mtu aliyesukuma ubomoaji huo kufanyika. Lakini jambo dhahiri ni kwamba jengo likishaporomoka hakuna tunachoweza kufanya na sijawahi kupoteza. Hata mambo yanapoharibika sipotezi maana Mungu ana mpango wake,” aliongeza mwanamuziki huyo.

Hata hivyo alifichua mipango yake ya kununua mali nyingine huko Dandora na katika mtaa wowote mwingine jijini Nairobi.

Mnamo Juni 23, 2024, baada ya agizo kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kituo cha mwanamuziki huyo kilichokuwa kwa jengo la orofa mbili kilibomolewa.

Lengo la serikali katika ubomoaji huo lilikuwa ni kuwahamisha watu wanaosihi karibu sana na mito kuepusha maafa kipindi cha mvua kubwa na mafuriko.