JUMA NAMLOLA: Bunge lisitumiwe kama ‘danganya toto’ kuwapa wananchi matumaini hewa

JUMA NAMLOLA: Bunge lisitumiwe kama ‘danganya toto’ kuwapa wananchi matumaini hewa

Na JUMA NAMLOLA

KUNA hekaya maarufu sana miongoni mwa wakazi wa Pwani. Aliyekuwa Seneta wa Kwale, marehemu Boy Juma Boy (Mola amrehemu), aliisimulia hekaya hii wakati wa uhai wake kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Simba alikuwa rafiki mkubwa wa nyani. Alipohisi njaa, akamtaka rafikiye apande juu ya mti aangalie kama kulikuwa na hatari yoyote au mambo yalikuwa shwari. Nyani ndiye anayeweza kukwea mitini au hata kuruka kutoka mti mmoja hadi mwingine kwa urahisi. Ule mti ulikuwa mgunga, wenye miba mirefu.

Nyani alipanda kwa uangalifu lakini miiba ilimdunga, akatiririkwa na damu. Simba pale chini ya mti, aliilamba damu kwa furaha. Nyani kuangalia chini, akamwambia simba, “Nimeangalia kote sijaona jambo.

Jambo lipo hapa nilipo.”Wakenya walipopandishiwa bei ya mafuta Septemba 15, kulikuwa na vilio kutoka kila pembe ya nchi. Wabunge kupitia kamati ya Fedha, walijikusanya na kuangalia upya mswada wa Fedha, uliosababisha kupanda kwa bei ya mafuta na gharama ya maisha kwa jumla.

Kamati hiyo chini ya Mbunge Mwakilishi wa Kike Homa Bay, Gladys Wanga, iliwasilisha ripoti kwa Karani wa Bunge Oktoba 12. Miongoni mwa wengine, kamati hiyo ilipanga kufanyia marekebisho sheria ya ushuru, ili kuondoa baadhi ya kodi zinazosababisha bei ya mafuta kuwa juu.

Tangu Katibu wa Bunge apokee mapendekezo hayo na kuyaidhinisha yajadiliwe, mwezi mmoja umepita bila ya lolote kutangazwa kwa umma.Wabunge wamejushughulisha mno na kuwaandamana wanasiasa wanaotafuta urais, badala ya hili linalowahusu wananchi.

Bei mpya ya mafuta inapotarajiwa kuanza kutumika Jumatatu, ni dhahiri kuwa hakuna jipya . Mamlaka ya Kudhibiti kawi (EPRA) inapotathmini bei ya mafuta, huongozwa na kanuni na sheria. Ili kubadili chochote, ni lazima wabunge washiriki.

Katika muktadha wa sasa ambapo mswada hubaki kwa siku 90 pekee, kuna uwezekano mkubwa kwamba kelele za kamati ya Bi Wanga zilikuwa ni ‘danganya toto’.

jnamlola@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Rais akamatwa

Uingereza yaahidi kupiga jeki uchumi wa Kenya

T L