Afya na Jamii

Jumbe za pesa husaidia wanaume wanene kupunguza uzani wa mwili

May 20th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

MAZOEZI yamekuwa yakifahamika kama suluhu kwa wanaume ambao ni wanene kupita kiasi na walio na mafuta mengi mwilini.

Katika kile ambacho kitawafurahisha wengi, utafiti umebaini kuwa wanaume wanene wakitumiwa pesa ili kupunguza uzani, wanafanikiwa kupunguza kilo hizo.

Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la JAMA Network Uingereza umebaini kuwa wanaume wenye unene kupita kiasi hupunguza kilo, wakilipwa kwa kutumiwa pesa kwenye simu zao mara kwa mara.

Lengo la kutumiwa pesa ni jumbe hizo kuwashaajisha wapunguze kilo ikizingatiwa wengi hupokea kwa furaha jumbe za kutumiwa pesa kama tunu.

Unene kupita kiasi huhusishwa na kisukari, saratani na magonjwa ya moyo.

Utafiti huo ulibaini kuwa kawaida wanaume huwa hawashiriki vipindi vya mazoezi kupunguza uzani wao ikilinganishwa na wanawake.

Hii ndiyo maana lazima kutumike njia nyinginezo za kuwasaidia kupunguza uzani mwilini ili kuwa imara kiafya ikiwemo kutumiwa pesa.

Utafiti huo uliwashirikisha wanaume wanene ambao walipewa maagizo ya kufuata kupunguza uzani mwilini mwao ikiwemo mazoezi na mtindo wa kula huku wakifuatiliwa na kutumiwa hela kulingana na kiwango cha kilo ambazo kila moja alikuwa amepunguza.

Wale ambao walipunguza uzani wao kwa kiasi cha juu watumiwa donge nono kwq simu na wale ambao hawakupunguza, walitoka mikono mitupu.

Baada ya miezi 12, asilimia kubwa ya wanaume ambao waliyafuata maagizo na kubadilisha mtindo wao wa kula, walikuwa wamepunguza uzani na kunufaika na hela zilizokuwa zikitolewa.

Wale ambao hawakuyafuata maagizo yote lakini wakajizatiti pia walipunguza unene japo kiasi na wakalipwa kwa kiwango chao.

Hata hivyo, walioendelea na maisha yao ya kawaida bila kushiriki juhudi zozote walisalia na wanene na kutofaidika.

Ingawa hivyo, ila ya utafiti huu ni kuwa baadhi ya wanaume ambao ni matajiri hawakushiriki au kushughulishwa na ahadi ya pesa.

Waliolengwa sana ni wale ambao huwa na mapato ya kadri au ya chini na wana unene kupita kiasi.

Hata hivyo, ni bayana kuwa jumbe za pesa zina mchango mkubwa katika kuwasaidia wanaume wenye unene kupita kiasi kupunguza uzani wao.