Makala

Jumbe za pongezi Raila Odinga akitimiza miaka 79

January 7th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKENYA na viongozi mbalimbali Jumapili, Januari 7, 2024 waliungana pamoja kumtumia jumbe za heri njema kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kwa kutimiza miaka 79 tangu kuzaliwa kwake.

Baadhi ya viongozi waliomtumia Bw Odinga jumbe hizo ni kiongozi wa chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua, Kalonzo Musyoka (Wiper), chama chake cha ODM, mbunge Kanini Keega (Bunge la Afrika Mashariki-EALA), Seneta Edwin Sifuna wa Nairobi kati ya wengine.

“Siku njema ya kuzaliwa kinara wangu Raila Odinga. Nakutakia maisha marefu,” akasema Bi Karua kupitia mtandao wa X.

Akasema Bw Musyoka: “Heko Bw Odinga unaposherehekea siku yako ya kuzaliwa. Kuna watu wachache waliojitolea kuitetea nchi kama wewe.”

Kwenye taarifa, chama cha ODM kilisema: “Tunajiunga na Wakenya na dunia nzima kumtakia kiongozi wetu, Bw Raila Odinga, afya nzuri na baraka anaposherehekea siku ya kuzaliwa leo. Kama chama, tunajivunia kuwa sehemu ya safari yake ya ufanisi mkubwa. Siku njema ya kuzaliwa!

Akasema Bw Sifuna: “Siku njema ya kuzaliwa ‘Baba’ Raila Odinga! Sisi ni wale tuliobarikiwa, tukakujua nawe ukatujua. Ahsante kwa yote unayoendelea kulifanyia taifa letu. Mungu akulinde na akupe maisha marefu.”

“Heko kwa siku ya kuzaliwa ‘Baba’ Raila Odinga. Mungu akupe maisha marefu!” akasema Bw Kega.

Bw Odinga alizaliwa mnamo Januari 7, 1945.

Wazazi wale walikuwa Mary Juma Odinga na mwanasiasa Jaramogi Oginga Odinga katika Kaunti ya Kisumu (wakati huo ikiwa wilaya).