Habari MsetoSiasa

Jumla ya Wakenya 213,000 watazama mwili wa Moi

February 10th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya Wakenya 213,000 walipata fursa ya kutizama mwili wa Rais wa zamani Marehemu Daniel Arap Moi shughuli hiyo ilipokamilisha mwendo was aa kumi na mbili jioni Jumatatu.

Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Spika wa Bunge Justin Muturi na ambayo ilinaswa kwenye mitambo ya kieletroniki langoni mwa majengo ya bungeni.

Shughuli ya kutizama mwili huo ilianza Jumamosi Februari 8, mwendo wa nne za asubuhi na kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na mkewe Margaret Kenyatta.

Serikali ilitenga siku tatu kwa Wakenya kufika katika majengo ya bunge kutoa heshima zao za mwisho kwa rais huyo wa Jamhuri ya Kenya ambaye aliongoza kwa miaka 24.

Foleni ndefu za Wakenya waliokuwa na hamu ta kutoa heshima zao kwa Mzee Moi zimeshuhudiwa jijini Nairobi kwa siku tatu kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa walisema kuwa walisafiri kutoka maeneo ya mbali kufika Nairobi angalau wasiachwe nje katika shughuli hiyo ya kipekee na kihistoria.

“Mimi nimesafiri kutoka kaunti ya Kilifi kuja hapa mahsusi kuona mwili wa Rais niliyempenda zaidi Mzee Moi. Alikuwa kiongozi shupavu na aliyependa nchini yake,” Bw Brian Charo, 40, akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Miongoni mwa watu waliofika kutizama mwili wa marehemu ni watumishi wa umma waliostaafu na ambao walifanya kazi chini ya utawala wa Mzee Moi.

Awali, baadhi ya Wakenya waliokuwa wamepiga foleni walionekana kulemewa na joto kutokana na jua kali na kupewa huduma na wahudumu wa Shirika la Msalaba Mwekundu na lile la St John Ambulanse.