Habari

Jumwa akalia kaa la moto

October 20th, 2020 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Malindi, Aisha Jumwa pamoja na msaidizi wake, Geoffrey Otieno wataadhimisha sikukuu ya Mashujaa korokoroni.

Jumatatu, Mahakama Kuu ya Mombasa iliagiza kwamba, wawili hao wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Bandarini kwa siku tatu, huku wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kushtakiwa na kosa la mauaji.

Akitoa amri hiyo, Jaji Njoki Mwangi alielekeza wawili hao wapelekwe hospitalini kesho (Jumatano) kutokana na kwamba leo ni Sikukuu ya Kitaifa.

Agizo la mahakama huenda likawa kaa la moto kwa Bi Jumwa, kwa kuwa matokeo ya aina yoyote yatakuwa na athari kwake. Iwapo daktari atathibitisha kuwa ana akili timamu, atalazimika kuingia kizimbani kujibu mashtaka kuhusiana na mauaji wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo mwaka jana.

Na iwapo atasemekana kuwa asiye na akili timamu kujibu mashtaka, kuna uwezekano wa kupelekwa katika Hospitali ya Wendawazimu na pia, kifungu cha 99(2)e cha Katiba kinasema hawezi kuendelea kuwa mbunge.

“Katika muda huo, afisa wa kurekebisha tabia anapaswa kuandaa ripoti kamili kuhusu washukiwa hao,” akasema Jaji Njoki.

Mahakama ilitoa amri hiyo baada ya upande wa mashtaka kulalamika kwamba, washukiwa hao walidharau amri ya kuwataka kufika hospitalini, kufanyiwa uchunguzi wa akili.

Kiongozi wa Mashtaka, Bw Alloys Kemo alisema kuwa, licha ya wawili hao kupata ujumbe wa kufika hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa akili, na wakaahidi kuwa wangefika katika hospitali kuu ya eneo la Pwani (CGPH), walikosa kufanya hivyo.

“Tunaomba washukiwa hao wazuiliwe gerezani ili kuwapa maafisa wa polisi muda wa kuchukua alama za vidole na taarifa zingine muhimu zitakazohitajika kortini,” akasema Bw Kemo.

Hata hivyo, washukiwa hao kupitia kwa wakili wao, Bw Jared Magolo walijitetea kuwa walikosa kufika hospitalini kwani ujumbe walioupata haukueleza ni wapi wangefanyiwa uchunguzi na muda wa kujiwasilisha.

Bi Jumwa na Bw Otieno wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Bw Jola Ngumbao, ambaye alikumbana na kifo chake mnamo Oktoba mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda.

Inasemekana kuwa Bw Ngumbao alipigwa risasi na kuaga dunia katika eneo la Mshongaleni Pendu Kiani, baada ya mbunge huyo na wafuasi wake kuvamia na kuzua vurugu katika mkutano wa kisiasa wa mwaniaji wa kisiasa wa chama cha ODM, Bw Reuben Katana ambaye ni Mwakilishi wa Wadi ya Ganda.

Hata hivyo, Bi Jumwa amekuwa akidai kwamba, mashtaka dhidi yake yanatokana na maamuzi yake ya kisiasa ya kuunga mkono Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.