Jumwa akwamilia UDA, adai Ruto ataingia Ikulu 2022

Jumwa akwamilia UDA, adai Ruto ataingia Ikulu 2022

Na VALENTINE OBARA

VIGOGO wa kisiasa ambao wangependa kumvuta Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa upande wao kutoka kwa kikosi cha Naibu Rais William Ruto kabla Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, huenda wakahitajika kujikakamua zaidi.

Mbunge huyo ambaye amepanga kuwania ugavana wa Kaunti ya Kilifi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, amepuuzilia mbali madai kwamba ameanza kunyemelea upande wa kisiasa unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Uvumi kuwa Bi Jumwa alipanga kuhama kundi la Tangatanga linaloongozwa na Dkt Ruto ulianza kuenea wikendi wakati alipokutana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli.

Ilifichuka kuwa, wawili hao pamoja na Mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader walikutana faraghani katika hoteli iliyo Kaunti ya Kilifi.

Baadaye, Bw Atwoli alikutana na Bw Odinga, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, mwenzake wa Rarieda Otiende Amolo na Seneta wa Siaya James Orengo katika kaunti hiyo ikadaiwa Bi Jumwa ndiye aliyewapiga picha iliyokuwa ikisambazwa mitandaoni.

Hata hivyo, Bi Jumwa alijitokeza Jumatatu katika mkutano wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachohusishwa na Dkt Ruto kusisitiza msimamo wake.

Mkutano huo ulioleta pamoja makundi ya wanawake wa eneobunge la Kiambaa ulikuwa wa kumpigia debe mpeperushaji tikiti ya UDA katika uchaguzi mdogo wa Juni 15, Bw John Njuguna Wanjiku.

Alitumia hotuba yake katika mkutano huo kusisitiza hana nia ya kubadili msimamo wake akiashiria kupanga kutumia UDA kuwania ugavana mwaka ujao.

“Nataka wajue Aisha Jumwa hataondoka katika UDA. Mimi si mpangaji katika UDA bali ni mmiliki. Tunaunda serikali ijayo wapende wasipende,” akasema.

Bi Jumwa ni miongoni mwa wanasiasa ambao walikuwa mstari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga kwa urais 2017, kabla ya kubadili msimamo.

Waasi wengi wa ODM pamoja na wengine wa Jubilee waliamua kujiunga na Dkt Ruto ambaye alianza kujitafutia umaarufu mapema akipanga kuwania urais kupitia UDA 2022.

Kwa upande wake, Bw Feisal aliwania ubunge katika uchaguzi mdogo Msambweni akiungwa mkono na kikosi cha naibu rais, akafanikiwa kushinda kiti hicho, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Suleiman Dori.

Kabla kufariki kwake, Bw Dori pia alikuwa ameanza kukiasi Chama cha ODM ambako alikuwa ni mwanachama.

Bw Atwoli alidokeza kuwa yeye ndiye aliyeitisha mkutano na wabunge hao wawili akathibitisha walijadiliana kuhusu masuala ya kisiasa.

Ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo yao, mikutano aina hiyo huashiria upangaji wa mikakati ya kisiasa wakati huu uchaguzi unapokaribia ndiposa ukaibua gumzo mitandaoni.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri kuhusu siasa bora zitakazofaidi nchi yetu na tumekubaliana kuhusu mambo mengi. Mimi ni mzee, huwa sialikwi katika mikutano bali mimi ndiye hualika watu,” akasema Bw Atwoli.

Bw Atwoli ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga licha ya kuwa mwanachama wa KANU, amejizolea sifa kwa kupanga mikutano ya kupatanisha wanasiasa wa pande tofauti hasa wanaojaribu kwenda kinyume na misimamo ya waziri huyo mkuu wa zamani.

Mkutano wake na wabunge hao wawili ulitokea wakati ambapo ODM imepoteza wabunge wengi na wanasiasa wengine Pwani, huku idadi ya wanachama wa Jubilee wanaoegemea upande wa UDA katika ngome za Rais Kenyatta ikizidi kuongezeka.

“Kuna watu walikuwa wanasukuma gurudumu la ODM Pwani na sasa hawapo. Jubilee na ODM zimeisha,” alisema Bi Jumwa katika mahojiano ya awali kwa kituo cha redio cha eneo hilo.

Hata hivyo, wanachama wa ODM wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama, wanasisitiza bado chama hicho kina umaarufu Pwani kinyume na jinsi wapinzani wao wanavyofikiria.

You can share this post!

KRU imani tele mashabiki wa raga watarejea viwanjani Desemba

CHARLES WASONGA: Walimu wakuu wanaoendelea kutoza ada za...