Jumwa amsifia Ruto, asema ndiye suluhu ya uchumi wa nchi uliodorora

Jumwa amsifia Ruto, asema ndiye suluhu ya uchumi wa nchi uliodorora

NA ALEX KALAMA

MGOMBEA ugavana wa kaunti ya Kilifi kupitia chama cha UDA ambaye ni mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amewataka wakazi wa Kilifi kupigia kura kinara wa muungano wa Kenya Kwanza, Dkt William Ruto kuwa rais wa tano akisema ana mipango ya kuwakomboa kutoka hali ngumu ya maisha wanayopitia kwa sasa.

Akizungumza katika wadi ya Kibarani eneo bunge la Kilifi Kaskazini, Bi Jumwa amewataka wakazi wa Kilifi kutomuunga mkono Odinga kuwa rais akidai alichangia hali ya uchumi iliyo kwa sasa.

“Mwaka wa 2013 hadi 2017 wakati mshauri wa rais alikuwa Ruto bei ya unga ilikuwa nafuu. Uhuru alipompiga teke na kumwambia ‘wewe hufai nimepata mshauri anaitwa Raila Odinga’ bei ya unga imefika Sh250. Halafu Uhuru Kenyatta anasema nyinyi Wakenya mmpigie Raila kura aendeleze kazi yake,” alisema Bi Jumwa.

Kwa upande wake mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya alimpigia debe Ruto na kuwaahidi wakazi wa Kibarani kwamba atashughulikia maskwota wa shamba la Kiwapa kwa kununua shamba hilo na kuwapatia wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo hiyo mwaniaji wa kiti cha Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi kupitia chama cha Kadu Asili, Ephie Chari amewataka wakazi wa kaunti hiyo kufanya uamuzi bora wakati wa uchaguzi mkuu ujao na kuchagua mtu binafsi wala sio chama.

You can share this post!

Mikakati ya Nassir kufufua uchumi Mombasa

Chipukizi wa Uingereza U-19 wazamisha Israel na kutwaa taji...

T L