Jumwa aonywa UDA itazima nyota yake

Jumwa aonywa UDA itazima nyota yake

Na ALEX KALAMA

WABUNGE wa chama cha ODM wamemwonya Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa kwamba, nyota yake ya kisiasa iko hatarini kuzima baada ya kuamua kuungana na Naibu Rais William Ruto.

Wakiongea katika eneo la Dabaso, Kaunti ya Kilifi Jumanne, walisisitiza ODM bado ndio maarufu katika kaunti hiyo licha ya Bi Jumwa kusisitiza imepoteza umaarufu.

“Nataka kuwaambia wale viongozi ambao wasema ODM imefifia hapa Kilifi wanajidanganya. Mimi kama naibu mwenyekiti wa ODM hapa Kilifi nina imani kwamba hata 2022 bado serikali Kilifi itakuwa ya ODM. Kwa sababu chama hiki ndicho chenye maono bora, waacheni wapige kelele wanapoteza muda wao bure,” alisema Bw Mwambire.

Bi Jumwa ametangaza azma ya kuwania ugavana Kilifi mwaka ujao kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Viongozi hao walikuwa katika mazishi ya Japhet Kabenge Mung’aro ambaye ni mjomba wa Waziri Msaidizi wa Ugatuzi Gideon Mung’aro.

Bw Mung’aro ameashiria nia ya kujiunga na ODM kuwania ugavana mwaka ujao, na anatarajiwa kupigania tikiti ya chama hicho dhidi ya Naibu Gavana Gideon Saburi.

Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed alitaka wakazi wa Kilifi wajiulize ni maendeleo gani ambayo Bi Jumwa amefanikiwa kuleta katika eneobunge la Malindi tangu alipoasi ODM, ikilinganishwa na wabunge waliobaki ndani ya chama.

“Wajua huyo Aisha mimi namuonea huruma. Huwezi kuzungusha kiuno bila manufaa yoyote, hiyo ni hasara kubwa kwa watu wa Kilifi,” alisema Bw Mohamed.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga pamoja na wanasiasa wengine akiwemo Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Seneta Maalumu wa Jubilee Christine Zawadi miongoni mwa wengine.

You can share this post!

Jaji aliyetimuliwa adai alitemwa bila utaratibu

Eid: Viongozi wavunja desturi ya Kiislamu sababu ya siasa