Jumwa apuuza hitaji la digrii kwa uongozi wa kisiasa

Jumwa apuuza hitaji la digrii kwa uongozi wa kisiasa

Na MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa amepuuzilia mbali suala la kuwa wanasiasa watahitajika kuwa na digrii kuwania viti katika uchaguzi ujao.

Akizungumza akiwa Kilifi, Bi Jumwa alisema sehemu hiyo ya sheria itarekebishwa kabla ya uchaguzi, hivyo wanasiasa waendelee kujipigia debe na kuwaachia wapigakura nafasi ya kujichagulia kiongozi wanayemtaka.

“Msiwe na wasiwasi kuhusu hitaji la kuwa na digrii kabla ya kushiriki uchaguzini. Sehemu hiyo itafanyiwa marekebisho na wapigakura wataamua viongozi wanaotaka,” akasema.

Hata hivyo, aliwashauri wanasiasa wahakikishe kuwa vyeti vyao vya elimu ni halali kutoka kwa taasisi za elimu zilizosajiliwa ili wajiepushie matatizo wanapofuata maazimio yao ya kisiasa.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw Nelson Dzuya alikuwa amedai kuwa mapendekezo ya kurekebisha katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) yakipitishwa, hakuna kiongozi atakayechaguliwa kama hana shahada ya digrii.

Alipokuwa akizungumza katika eneobunge la Rabai, Bw Dzuya alisema pendekezo hilo litahakikisha kuna viongozi wanaoelewa majukumu yao bungeni kuanzia kwa madiwani hadi maseneta.

Aliwaonya baadhi ya wanasiasa ambao wameanza kampeni mapema kwamba huenda majina yao yakakosekana katika karatasi za kura kwa sababu hawana kiwango cha kutosha cha elimu kitakachohitajika.

“Kila wakati matokeo ya KCPE na KCSE yanapotangazwa, idadi kubwa ya watahiniwa hupata matokeo mabaya na huwa tunaambiwa waliopata alama za A na A- wataongozwa na wale waliopata D kwa sababu ndio wanasiasa wa kizazi kijacho,” akalalama Bw Dzuya.

You can share this post!

Ronaldo avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye soka ya...

Ufaransa wang’aria Ujerumani kwenye gozi kali la Euro