Habari MsetoSiasa

Jumwa ashangaza kusema Ruto ndiye 'Mungu'

May 20th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

VIBARAKA wa kisiasa wapo lakini mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amewaacha Wakenya kwenye mshangao. Hii ni baada ya kummiminia sifa Naibu Rais Dkt William Ruto, wakati huu akimweka kiwango sawa na Mungu.

Katika hafla iliyokuwa eneo la magharibi, Bi Jumwa ambaye sasa amekuwa mwandani mkubwa wa Dkt Ruto kwa miezi kadhaa alionyesha hadharani kiwango ambacho yuko tayari kumfurahisha Naibu Rais.

Hii ni aliposema hakuna anayefanana na Naibu Rais na hata akageuza wimbo wa kumsifu Mwenyezi Mungu, akiondoa jina la Mungu na kuweka lile la Ruto.

“Mimi nimemwangalia Naibu Rais kutoka Pwani hadi huku, yale mambo anafanya…ukitaka barabara-Ruto yuko pale, makanisa kujengwa-Ruto yuko hapo, ukitaka shule kujengwa, mabasi ya watoto kununuliwa, ukitaka maji-Ruto yuko pale. Ni nani anayefanana na Ruto?” mbunge huyo akasema akihutubia hadhira.

Hakumalizia hapo ila aliendelea kuuimba wimbo wa kikristo, japo badala ya kuwa na jina la Mwenyezi Mungu, akatia jina la Dkt Ruto.

“Hakuna wa kufanana na Ruto…Ruto aweza..Ruto atenda…hakuna wa kufanana naye,” Bi Jumwa akaongoza hadhira kuimba.

Huenda wengi walikuwa wamedhani kugura chama cha ODM na kujipiga kifua kuwa yuko tayari kukabiliana nao kwa msaada wa Dkt Ruto ndicho kilikuwa kiburi cha juu zaidi kwa Bi Jumwa, lakini sasa kumsifu kiwango sawa na Mungu kimewaacha wengi vinywa wazi.

Matukio hayo aidha yametokea wakati Naibu Rais amekuwa akitumia kila mbinu kuvuta makanisa na viongozi wa dini upande wake, madai kuwa huenda anajaribu kutumia pesa zake kujipendekeza kwa Mungu yakizidi.

Lakini Dkt Ruto mbeleni alisema kuwa “sisi tunawekeza mbinguni” kuwakabili wanaomkosoa kwa kumkaribia Mungu, japo sasa inaonekana kwa wafuasi wake amemfikia Mungu na kuanza kumwondoa kutoka kiti chake.