Jumwa ashindwa kushawishi mahakama iahirishe kesi yake ya tuhuma za ufisadi

Jumwa ashindwa kushawishi mahakama iahirishe kesi yake ya tuhuma za ufisadi

Na PHILIP MUYANGA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa pamoja na washukiwa wengine sita wa ufisadi walilazimika kujibu mashtaka licha ya mawakili wao kusema wamejiondoa katika kesi hiyo.

Mawakili walijiondoa baada ya Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bi Edna Nyaloti kukataa kuahirisha kesi hiyo.

Walitaka iahirishwe wakati upande wa mashtaka ulipobadilisha hati ya mashtaka na wakasema walihitaji muda kushauriana na wateja wao kuhusu mabadiliko yaliyofanywa.

Mabadiliko hayo yanahusu nambari ya zabuni ambayo ilitolewa na afisi ya Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maendeleo katika Maeneobunge eneo la Malindi (NG-CDF).

Bi Nyaloti aliwaruhusu mawakili Danstan Omari, Jared Magolo, Titus Kirui na Shadrack Wambui waondoke mahakamani baada yake kuagiza kuwa Bi Jumwa na washtakiwa wenzake wajibu mashtaka.

“Sehemu 214 ya taratibu za kesi ya uhalifu inaruhusu upande wa mashtaka kufanyia marekebisho hati ya mashtaka,” akasema Bi Nyaloti.

Baada ya kutoa uamuzi huo ndipo mawakili walisema hawatawakilisha washtakiwa katika kesi hiyo.

“Hatuko tayari kuendelea mbele. Tuna maagizo tujiondoe sote katika kesi hii,” akasema Bw Omari.

Mawakili walisema hawana uwezo kuendelea kuwakilisha wateja wao ipasavyo bila kupewa maagizo nao kuhusu mabadiliko yaliyofanywa.

Washtakiwa walikanusha mashtaka hayo yaliyo katika hati mpya ya mashtaka.

Mawakili walidai kuwa walipopewa hati mpya ya mashtaka siku kadhaa zilizopita, walishindwa kuwapata washtakiwa ili washauriane kuhusu marekebisho yaliyofanywa.

Bw Omari alisema marekebisho yalikuwa yamefanywa katika nambari ya zabuni na hivyo basi walihitaji mwelekeo mpya kutoka kwa wateja wao.

Upande wa mashtaka ulikiri kuwa nambari ya zabuni katika hati ya awali ilikuwa tofauti na ile iliyo katika hati mpya lakini tofauti ni katika herufi mbili pekee.

Viongozi wa mashtaka, Bw Henry Kinyanjui na Bw Alex Akula walieleza hapakuwa na jambo lolote jipya lililobadilika isipokuwa herufi hizo, na stakabadhi zote zinazotumiwa zilitoka kwa washtakiwa.

Bi Jumwa ameshtakiwa kwa madai ya kushiriki katika njama ya ufisadi wa Sh19 milioni zilizolipwa kwa kampuni ya Multiserve kupitia kwa zabuni nambari MLD/NG-CDF/01/2017/2018 iliyotolewa na afisi ya CDF ya Malindi.

Washtakiwa wenzake ni Wachu Omar, Kennedy Otieno, Bernard Riba, Sophia Saidi, Margaret Kalume, Robert Katana na kampuni ya Multiserve.

Imedaiwa kuwa kitendo hicho kilitokea kati ya Mei 14 na Oktoba 12, 2018 katika Kaunti Ndogo ya Malindi, Kaunti ya Kilifi.

You can share this post!

KEG yatangaza tarehe za mjadala wa kuwaleta jukwaa moja...

Pigo Barcelona jeraha likitarajiwa kumweka nje Aguero kwa...