NA MAUREEN ONGALA
WAZIRI wa Utumishi wa Umma na Jinsia, Bi Aisha Jumwa, amefafanua kwamba hatua yake ya kushirikiana na Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, haimaanishi kwamba ameweka kando azimio la kuwa gavana wa kaunti hiyo katika miaka ijayo.
Katika siku za hivi majuzi, wanasiasa hao wawili wamekuwa wakihudhuria hafla mbalimbali katika Kaunti hiyo kwa pamoja huku wakisema uamuzi wao wa kushirikiana ni kwa azma ya kuletea wakazi maendeleo.
Kulingana na Bi Jumwa, viongozi wa Kilifi wameamua kwamba watashirikiana na Bw Mung’aro ili atimize ajenda zake kwa watu wa Kilifi bila kutatizwa.
“Gavana Mung’aro alitupa manifesto yake na sasa ni wakati wa kumuunga mkono ili baada ya miaka mitano aje kusimama mbele yetu tena atueleze mafanikio yake. Sijasema kuwa ndoto yangu ya kuwa gavana wa Kilifi imekufa, imeahirishwa tu ikingoja wakati muafaka,” akasema.
Viongozi wa Kilifi walitoa wito kwa wakazi wa Kilifi kumpa gavana Bw Mung’aro nafasi nzuri ya kufanya kazi.
Walieleza kuwa hatua ya baadhi ya watu kuenda kortini kumzuia Bw Mung’aro kutekeleza baadhi ya majukumu yake itaathiri utendakazi wake.
Bw Mung’aro anakumbwa na kesi mahakamani inayopinga uteuzi wa maafisa wakuu 24 wa kaunti na nyingine inayopinga ushindi wake katika uchaguzi uliopita.
“Kuna watu wengi ambao wanamsumbua gavana Mung’aro. Nataka niwaeleze ndugu zangu, tukiendelea na mambo ya kortini kila wakati watakaoumia ni wananchi wa Kilifi na wala si Mung’aro au madiwani. Ni wananchi watakosa huduma mashinani,” akasema mbunge wa Ganze, Bw Kenneth Kazungu.
Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, aliwaomba waliowasilisha kesi dhidi ya Bw Mung’aro waziondoe.
Kauli sawa na hiyo ilitolewa na mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana. Hata hivyo, Bw Mung’aro alisema atasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu kesi zote dhidi yake.
“Nitaipa mahakama wakati ifanye kazi yake lakini nina imani kuwa itawapa watu wa Kilifi haki yao,” akasema.
Alisema kuwa kesi hizo hazitamzuia kuwahudumia wakazi wa Kilifi.
Subscribe our newsletter to stay updated