Jumwa atangaza kikosi chake 2022

Jumwa atangaza kikosi chake 2022

VALENTINE OBARA na KALUME KAZUNGU

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa ametangaza baadhi ya wanasiasa anaonuia kuungana nao anapolenga kuwania ugavana wa Kilifi mwaka ujao.

Bi Jumwa ambaye ni mwandani wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto, ni mmoja wa wanasiasa ambao walitangaza mapema mpango wa kushindania urithi wa kiti cha Gavana Amason Kingi.

Bw Kingi anatumikia kipindi chake cha pili cha uongozi kilicho cha mwisho kikatiba. Akizungumza katika hafla ya kijamii Kilifi mnamo Jumapili, Bi Jumwa alisema ameamua kuungana na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, mwanasiasa Juliet Baya almaarufu kama ‘Kachawawa’ anayepanga kuwania wadhifa wa mbunge mwakilishi wa kike kaunti, na afisa mkuu wa ujenzi, barabara na uchukuzi katika serikali ya Kaunti, Bw Kenneth Charo almaarufu kama ‘Tungule’ anayetarajiwa kuwania ubunge Ganze.

Hata hivyo, Bi Jumwa hajatangaza atamuunga nani mkono kwa wadhifa wa useneta akidai hakuna mwanasiasa anayetaka kiti hicho aliyemwendea kufikia sasa kutafuta ushirikiano naye.

“Orodha ya majina ya wale niliowataja ni kwamba wote tayari tushakaa chini na kujadiliana na kuafikiana mambo ni chonjo kwa kura ya 2022,” akasema.

Katika hafla hiyo, Bw Baya alisisitiza uaminifu wake kwa Bi Jumwa huku akipuuzilia mbali wanasiasa wengine anaodai wameanza kumwandama wakitaka awaunge mkono kwa ugavana mwaka ujao.“Nataka wajue kwamba wamechelewa. Mipango imekamilika.

Tumeamua ni William Samoei Ruto kwa urais, gavana wetu atakuwa Aisha Jumwa na nitakuwa mbunge wa Kilifi Kaskazini,” akasema.

Alisema nia yao ni kuhakikisha kuna mabadiliko Kilifi kuliko jinsi ilivyo sasa.Bi Jumwa ambaye alihudumu kama mbunge mwakilishi wa kike kaunti kati ya mwaka wa 2013 hadi 2017, ni miongoni mwa wanawake wachache Pwani ambao wameonyesha maazimio ya kutaka kuwania ugavana katika kaunti zao.

Wengine ni Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko (Mombasa), na mtaalamu wa masuala ya kijamii, Bi Umra Omar (Lamu).

Bi Jumwa anatarajiwa kushindania kiti hicho dhidi ya Naibu Gavana Gideon Saburi, Waziri Msaidizi wa Ardhi Gideon Mung’aro na Mbunge wa Magarini Michael Kingi miongoni mwa wengine.

Bw Baya ambaye awali alionyesha azimio kuwania ugavana alibadili nia wiki chache zilizopita na kuamua kumuunga mkono Bi Jumwa.

Wawili hao ni miongoni mwa wabunge waliokaidi Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, wakaamua kuungana na Dkt Ruto.

Hata hivyo, haijajulikana wazi watatumia vyama vipi mwaka ujao.Dkt Ruto tayari amedhihirisha nia ya kutumia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) anapojikakamua akiazimia kurithi kiti cha Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Tumjuavyo huyu Kalonzo, atakunja mkia tu

Raila akosoa ushuru wa juu unaotozwa wawekezaji