Habari Mseto

Jumwa kukamatwa kwa tuhuma za ufisadi

August 27th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameamuuru kukamatwa kwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa kwa madai ya kuhusika katika wizi wa Sh19 milioni fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF).

Tayari maafisa sita wa afisi ya CDF ya Malindi, ambao pia wanakabiliwa na tuhuma hizo, wamekamatwa na maafisa kutoka kitengo Idara ya Upelelezi ya Jinai (DCI) huku Bi Jumwa akiendelea kusakwa.

Wao ni pamoja na; Wachu Omar Abdalla (Meneja wa akaunti ya CDF ya Malindi), Kennedy Otieno Onyango, Benard Riba Kai, Sophia Saidi Charon na Margaret Faith Kalume ambao ni wanachama wa Kamati ya Zabuni ya Eneobunge la Malindi.

Mingine ni Robert Katana Wanje ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya Multserve Ltd.

Kulingana na DPP, Jumwa alitumia ulaghai kupokea fedha za umma kupitia kampuni hiyo ya ujenzi ambayo ilikuwa imepewa zabuni ya ujenzi wa Afisi ya Elimu katika kaunti ndogo ya Malindi.

“Multserve Contractors Limited ilipokea Sh19 milioni ambapo Sh2.5 milioni ilitumwa kwa Mheshimiwa Aisha Jumwa Karisa Katana ambaye ni Mbunge wa Malindi. Hii ni kielelezo wa mgongano wa masilahi,” akasema Bw Haji.

Kulingana na DPP, Jumwa alitumia fedha hizo, ambazo zilitokana na uhalifu, kununua nyumba kando la barabara ya Argwings Kodhek, Nairobi.

Mbunge huyo pamoja na watu hao sita watashtakiwa kuwa kosa la kupanga njama ya kutekeleza uhalifu, kutozingatia sheria za ununuzi wa bidhaa za umma, mgongano wa masilahi, ulanguzi wa fedha, kati ya makossa mengineyo.