Jumwa sasa amrukia Ruto mvutano na Kingi ukizidi

Jumwa sasa amrukia Ruto mvutano na Kingi ukizidi

NA MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, sasa anamtaka Naibu Rais, Dkt William Ruto, kuweka wazi mkataba kati ya muungano wa Kenya Kwanza na chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Hii ni kufuatia mvutano ambao umeibuka Kaunti ya Kilifi baina ya wanachama wa UDA wakiongozwa na Bi Jumwa, na PAA inayoongozwa na Gavana Amason Kingi ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

Miongoni mwa masuala yaliyobainika kuzua mvutano ni usimamizi wa kampeni za urais za Dkt Ruto, na ushindani wa viti kati ya wagombeaji wa UDA na PAA kuelekea kwa uchaguzi wa Agosti.

Bi Jumwa ambaye amepanga kuwania ugavana Kilifi kupitia UDA, amelalamika kuhusu uvumi na habari anazosema ni za kupotosha zinazoenezwa mashinani na kutatiza kampeni za UDA.

“Tunamwambia naibu wa rais, ambaye pia ni kinara wa chama chetu cha UDA kwamba aweke wazi makubaliano kati ya PAA na Kenya Kwanza ili tuweze kufanya kampeni zetu bila fujo,” akasema alipohudhuria mkutano wa wanawake.

Baada ya PAA kutangaza rasmi kujiunga na Kenya Kwanza, Dkt Ruto na Bw Kingi walijisifu kuwa, tofauti na mkataba wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambapo PAA ilihama, kulikuwa na uwazi katika Kenya Kwanza.

Alifafanua kwamba, kutakuwa na mashauriano kuhusu maeneo ambapo chama hicho kinaweza kukubaliana na UDA kuachia mgombeaji mmoja ili kusiwe na mgawanyiko wa kura za Kenya Kwanza.

Mpango huo ulinuiwa kufanywa kwa kuzingatia matokeo ya kura za maoni kuhusu umaarufu wa wagombeaji waliopewa tikiti za vyama hivyo.

Wiki iliyopita, Bw Kingi alisisitiza PAA itaendelea kuwa na wagombeaji viti kuanzia udiwani hadi ugavana.Kulingana na Bi Jumwa, matukio haya yametoa mwanya wa wafuasi wa UDA kuhadahiwa na chama cha PAA ili kuwaunga mkono katika uchaguzi ujao.

“Kilifi ni ngome ya UDA na wagombea viti wa UDA ndio watakaoibuka washindi katika uchanguzi mkuu wa Agosti 9,” akasema.

Vile vile, mbunge huyo alisema hakuna jinsi PAA inaweza kujitwika jukumu la kusimamia shughuli za Kenya Kwanza katika Kaunti ya Kilifi.

“Hakuna hata siku moja ambapo mpangaji anakuwa na kibali cha kuwa yeye ndiye mwenye nyumba,” akasema.

Hata hivyo msemaji wa chama cha PAA, Bw Lucas Maitha, alisema PAA kiko katika muungano wa Kenya Kwanza kama mshirika na haitatoa wawaniaji viti wake kwa sababu ya UDA.

Alieleza kuwa naibu rais alifahamu kuwa kuna maeneo ambayo UDA walikuwa wameweka wawaniaji viti hafifu na kunahitajika wagombeaji wenye nguvu kwa manufaa ya Kenya Kwanza.

“Tunalojua ni kuwa PAA iliweka mkataba na Kenya Kwanza, wala sio UDA na tumekuja na raslimali na watu wetu kusaidia muungano huo kushinda katika uchaguzi mkuu ujao,” akasema.

Bw Maitha alimtaka Bi Jumwa kuendeleza siasa za kuuza sera zake ikiwa anataka kupata ushindi wa ugavana.PAA ilimsimamisha Bw George Kithi, kuwa mgombeaji wake wa ugavana Kilifi huku ikiwa pia na wagombeaji viti vingine mbalimbali katika kaunti nyinginezo.

Mbali na Bi Jumwa, mshirikishi wa UDA katika Kaunti ya Kilifi, Bw Moses Matano, pia alisema ingelikuwa bora kwa naibu wa rais kuweka mkataba huo wazi ili wanachama wafahamu kuna ushirikiano aina gani baina yao na PAA katika Kenya Kwanza.

“Sisi kama wafuasi na wanachama hatukuwepo wakati wa makubaliano kati ya PAA na Kenya Kwanza, na ingekuwa vizuri iwapo tungefahamishwa yalimo katika mkataba huo,” akasema.

Alisema kuna uwezekano pia hali sawia inawakumba wafuasi na wanachama wa PAA ambapo hawajui kilichiko ndani ya mkataba huo na wako njia panda.

  • Tags

You can share this post!

Saburi akubali kuunga mkono Mung’aro kwa ugavana Kilifi

MWALIMU WA WIKI: Bi Wambui ni mwalimu kwa wito

T L