Siasa

Junet haendi popote, asema Raila

January 23rd, 2024 2 min read

NA STEPHEN ODUOR

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, amekanusha madai ya kuwepo kwa njama ya kumtimua mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed kutoka kwa chama hicho.

Akizungumza na wanachama wa ODM mjini Hola, Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya alisisitiza kwamba madai ya kutimuliwa kwa Bw Mohamed ambaye pia ni kinara wa wachache katika bunge yalikuwa propaganda zilizoenezwa na vyombo vya habari.

“(Junet) Mohamed haendi mahali popote. Kumekuwepo na porojo nyingi za magazeti. Katika nyumba kunaweza kuwa na tofauti ya maoni… hayo ni mambo ya kawaida,” akasema Bw Odinga.

Aliongezea kuwa Bw Mohamed hajaenda popote na wala hakuna yeyote aliyemgusa kwani angali mkurugenzi wa kampeni katika chama cha ODM.

Kauli ya Bw Odinga inajiri siku chache tu baada ya vyombo vya habari kuchapisha kwamba mbunge huyo wa Suna Mashariki aliitwa katika bodi ya maadili ya chama hicho kujitetea.

Huku taarifa hizo zikidokeza uwezekano wa kumvua mamlaka mbunge huyo iwapo atashindwa kujitetea na kujieleza kikamilifu.

Hata hivyo, Bw Odinga amekanusha kuwepo na nia na mipangilio kama hayo, akisema kuwa Bw Mohamed yupo na wala hakuna mpango wa aina hiyo.

Aidha, Bw Odinga amepuuzilia mbali ripoti za kuwepo kwa nyufa katika chama hicho, akisema kuwa ni madai ya “kufadhiliwa katika vyombo vya habari”.

Alisisitiza kwamba chama hicho kiko imara na kitaendelea kuwasajili wanachama ili kuendeleza uthabiti wake kwenye maeneo bunge na hata vijijini.

“Hizo ni njama za vyombo vya habari kuchochea tu vurugu katika chama, ni tabia isiyo nzuri. Kama chama tunaendelea kua na kuongezeka kwa idadi na shughuli hii itachangia zaidi nguvu yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa Azimio iko katika harakati za kuikomboa nchi kutoka kwa uongozi mbaya, huku akiwarai wakazi wa Tana River kukumbatia ndoto hiyo.

Kuitwa kwa Bw Mohamed na jopo la maadili katika chama cha ODM kulionekana kugawanya upinzani, baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho wakikosoa uamuzi huo.

Mbunge huyo wa Suna Mashariki hata hivyo hajaonekana katika hafla za chama kwa muda mrefu, huku baadhi ya wanachama wakionekana kumpiga vijembe katika mitandao ya X na Facebook kwa kudai kuwa alihujumu kampeni za Bw Odinga na hivyo kuchangia kushindwa kwake.

Bw Odinga aliandamana na Gavana wa Mombasa Mohammed Nassir, aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Seneta wa Kilifi Steward Madzayo na viongozi wengine katika kaunti.

Bw Nassir aliwarai wakazi wa Tana River kutafakari kwa kina “uongo mliouziwa na serikali ya Kenya Kwanza” na kuwataka kutumia busara katika siasa za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Nataka niwafumbue macho. Nyote mmeshuhudia mlioahidiwa na yale ambayo yamewakuta, toka hapa sasa na hata 2027 jiungeni na ODM na muanze kufanya maamuzi mazuri,” alisema Bw Nassir.

Katika shughuli hiyo ya usajili wa wanachama, ODM iliwapokea waliokuwa wanachama wa United Democratic Alliance (UDA).

Pia waliokuwa madiwani katika vyama vya Ford Kenya na Jubilee waliasi vyama vyao na kujiunga na ODM.