Habari MsetoSiasa

Junet: Ruto ni kama sisi, hajui lolote kuhusu muafaka, afyate ulimi

October 2nd, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

WABUNGE wa upinzani wamemtaka naibu wa Rais William Ruto kukoma kumshambulia kiongozi wao Raila Odinga na kukosoa muafaka baina yake na Rais Uhuru Kenyatta, wakimjulisha kuwa hakuwa sehemu ya muafaka huo.

Wabunge hao wamesema kuwa muafaka ulikua baina ya viongozi hao wawili pekee, na kuwa Bw Ruto ni abiria kwenye meli ya muafaka kama watu wengine tu, na hafai kujifanya kuwa miongoni mwa walioandaa muafaka huo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, wabunge hao walikosoa ziara za Bw Ruto nchini kila mara, ambazo amekuwa akimshambulia Bw Odinga.

“Awache kuzungumzia mambo ya muafaka kwani ulikua baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Hakuwa sehemu ya zoezi hilo, wala hatukumwona katika makao ya Harambee siku hiyo. Yeye si Rais wala hakuwa mgombea Urais mwaka jana na watu walienda debeni kuwapigia kura Raila na Uhuru,” akasema Junet.

Mbunge huyo ambaye ni mfuasi sugu wa Bw Odinga alisema watu wengine wote kando na Rais Kenyatta na Bw Odinga ni abiria, akiwemo Bw Ruto, akimtaka naibu wa rais kutumia mbinu zingine kupiga kampeni.

“Awache kutumia jina la Raila, hawezi kuifikia hadhi ya Bw Odinga, yale Raila ametimizia taifa hili yatamchukua Ruto miaka 50 kuyatimiza,” mbunge huyo akasema.

Alikuwa akizungumza pamoja na viongozi wengine wa upinzani ambao walimkabili Bw Ruto kwa kumshambulia Bw Odinga kuwa anataka kumwondoa Jubilee.