JUNGU KUU: Hatua ya Mudavadi inaweza kumponza

JUNGU KUU: Hatua ya Mudavadi inaweza kumponza

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuungana na Naibu Rais William Ruto imekuwa hasara kwake huku waliokuwa washirika wake wakihama chama hicho wakimlaumu kwa kupiga mnada jamii ya Mulembe.

Kuanzia Jumapili alipotangaza ushirikiano wake na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto, mibabe wa siasa kutoka Magharibi mwa Kenya ikiwemo kaunti yake ya nyumbani ya Vihiga waliokuwa wakimuunga mkono walijitenga naye wakisema kwamba hawatakubali jamii yao kupigwa mnada kisiasa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 unapokaribia.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa huenda hatua hiyo ikawa hasara kwa naibu waziri mkuu huyo wa zamani aliyekataa kuungana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye angali maarufu eneo la Magharibi.

Tayari wabunge na wanachama wa ANC wanaendelea kukihama kwa wingi na kujiunga na chama kipya cha Democratic Alliance Party Kenya (DAP-Kenya) kinachounga vuguvugu la Azimio la Umoja la Bw Odinga.

Miongoni mwa waliohama ANC baada ya Bw Mudavadi kuungana na Dkt Ruto ni mbunge wa Matungu Peter Namulindo, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende, mbunge wa Lugari Ayub Savula, Oku Kaunya wa Teso North, magavana, madiwani na wanasiasa kadhaa wenye ushawishi eneo hilo.

Bw Marende ambaye atagombea ugavana kaunti ya nyumbani ya Mudavadi ya Vihiga alitaja hatua ya Bw Mudavadi kama usaliti na kujitia kitanzi kisiasa katika juhudi za kupiga mnada jamii ya Mulembe.

“Ni hatua mbaya na Mudavadi alichofanya ni sawa na kujiua kisiasa kwa kujilipua kwa bomu,” alisema.

Kulingana na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, hatua ya Mudavadi ya kushirikiana na Dkt Ruto ni tukio la kutisha sio tu kwa jamii ya Mulembe pekee bali nchi kwa jumula.

Duru zinasema kuwa DAP Kenya na ODM vimeweka mikakati ya kufuta chembe za umaarufu wa ANC zilizobakia eneo la Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mikakati hiyo, aeleza Savula, itahusu kuandaa mikutano ya kufahamisha wakazi wa eneo la Magharibi mwa Kenya hatari ya Bw Mudavadi kushirikiana na Dkt Ruto.

“Tutapiga kambi eneo la Magharibi kuhakikisha Mudavadi anajuta kwa kupiga mnada jamii ya Mulembe. Tutaondoa kabisa uungwaji mkono ambao jamii ya Mulembe imesalia nao kwake. Hatutaruhusu jamii yetu kuuzwa kwa pesa chache na watu wawili kujaza matumbo yao,” alisema Bw Savula.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Bw Mudavadi huenda isimfaidi alivyotarajia hata baada ya kumvuta kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula katika ndoa yake ya kisiasa na Dkt Ruto.

“Lengo lake lilikuwa ni kugawanya kura za jamii ya Mulembe ambazo zimekuwa zikimwendea Bw Odinga mpinzani mkuu wa Dkt Ruto lakini jinsi hali ilivyo, huenda asifaulu,” alisema mdadisi wa siasa Peter Omamo.

Mchanganuzi huyu anasema kwamba hisia za wapigakura wa eneo la Magharibi ni kuwa Mudavadi na Wetangula walidanganywa na Dkt Ruto ili wamsaidie kumshinda Bw Odinga bila kujali maslahi ya jamii yao.

“Hali isipobadilika, na sioni ikibadilika sana, Mudavadi na Wetangula watabaki na viongozi wachache kama Malala ambao Mulembe inaamini walimsaidia kusaliti jamii yao,” asema Omamo.

You can share this post!

Ruto hatarini kwa ‘kubagua’ vyama vidogo Mlima Kenya

WALIOBOBEA: Beth Mugo: Aliacha alama katika sekta za Elimu,...

T L