Michezo

Junior Starlets kukita kambi Uhispania kwa mazoezi makali ya Kombe la Dunia

Na NA TOTO AREGE June 18th, 2024 2 min read

BAADA ya Junior Starlets kuandikisha historia kwa kuwa timu ya kwanza ya soka kutoka Kenya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia Jumapili, serikali imeweka mikakati ya maandilizi ya mapema kabla ya dimba hilo kufanyika Jamhuri na Dominica mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu.

Starlets walizima Burundi kwa jumla ya mabao 5-0 katika raundi ya nne na ya mwisho ya kuwania tiketi ya kufuzu barani Afrika.
Katika raundi ya kwanza Juni 8, Kenya ilishinda 3-0 nchini Ethiopia kabla ya kupata ushindi wa 2-0 katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi Jumapili.

Afrika itawakilishwa pia na Zambia na Nigeria.

Wenyeji Dominica, Brazil, Colombia, Ecuador, Uingereza, Japan, Korea DPR, Korea Kusini, Mexico, New Zealand, Poland, Uhispania, na Amerika ni timu nyingine ambazo zilifuzu.

Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), Nick Mwendwa, aliyehudhuria sherehe ya ushindi huo katika hoteli moja jijini Nairobi, alisema timu inatarajiwa kuondoka nchini Septemba kuelekea Mirabel, Uhispania, kwa mazoezi ya hali ya juu ya wiki tatu.

“Tulishirikiana pamoja na wizara za michezo na elimu kuhakikisha kwamba tunawapa wachezaji mazingira mazuri. Timu hii ikiondoka Uhispania, itaelekea Kombe la Dunia moja kwa moja,” alisema Mwendwa.

Wachezaji hao waliondoka kambini jana na kurejea shuleni kuendelea na masomo hadi Septemba.

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, ambaye aliongoza sherehe hiyo, alituza wanasoka hao Sh10 milioni. Katika kikosi hicho cha wachezaji 23 na maafisa 10 wa benchi la kiufundi, kila mmoja atapokea Sh300,000.

“Hongereni kwa kuiletea Kenya fahari kuandikisha historia. Ni thibitisho kwamba kuwekeza kupitia mpango wa Talanta Hela kunazaa matunda. Tutawapa sapoti ya kutosha kujiandaa kwa Kombe la Dunia,” aliongezea Ababu.

Kenya, Dominica, Ecuador na Poland zitashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa. Kombe hilo hufanyika kila baada ya miaka miwili. Litakuwa kila mwaka kuanzia mwaka 2025 likijumuisha mataifa 24. Morocco itaandaa makala 2025-2029.

Timu 16 zitakazoshiriki zitagawanywa katika makundi manne ya timu nne.

Timu mbili za kwanza katika kila kundi zitaingia robo-fainali. Hii itafuatiwa na nusu-fainali, mechi ya kuwania nafasi ya tatu na fainali.

Tarehe kamili ya droo hiyo bado haijatangazwa, lakini inatarajiwa kufanyika mwezi huu.