Michezo

Junior Starlets tayari kuvuruga Ethiopia Ijumaa

May 9th, 2024 2 min read

NA TOTO AREGE

TIMU ya taifa ya wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 (Junior Starlets) Ijumaa itakuwa ugenini jijini Addis Ababa kuvaana na timu ya taifa ya Ethiopia (The Animals) katika safari yake ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2024.

Mechi hiyo ya kwanza kwenye raundi ya tatu itachezewa Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, kuanzia saa tisa Alasiri.

Mechi ya marudiano imepangwa kufanyika Mei 19, 2024 jijini Nairobi katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex.

Kikosi hicho cha wachezaji 23 kikiongozwa na kocha Mildred Cheche, kiliwasili nchini Ethiopia Jumatano usiku na kufanya mazoei ya mwisho katika uwanja huo wa Abebe Bekila Alhamisi jioni.

Kenya na Ethiopia hazijawahi kukutana katika kiwango hiki, lakini kuelekea mechi hii, Ethiopia ndio wanaojivunia uzoefu mkubwa katika mashindano haya wakilinganishwa na Kenya ambayo hii ni mara ya kwanza kushiriki.

Wenyeji waliinyoa Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-0 kufuatia sare ya 0-0 na ushindi wa 3-0 ugenini na nyumbani mtawalia mwezi Februari katika mikondo miwili.

Kenya ilipangwa kucheza dhidi ya Jamhuri ya Kongo (DRC) katika raundi ya pili mwezi huo wa Februari, lakini wapinzani hao wakajiondoa, na kuwachia Kenya kusonga moja kwa moja hadi raundi ya tatu.

Mshindi wa jumla atafuzu kwa raundi ya nne ambayo ni ya mwisho kabla ya kukutana na mshindi wa mechi kati ya Djibouti au Burundi ambazo pia zinakabana koo leo.

Mshindi katika raundi hiyo ya mwisho atapata tikiti ya moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake mnamo Oktoba 2024, nchini Jamhuri ya Dominika.

Valarie Nekesa ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho ataongoza mashambulizi akisaidiwa na Marion Musanga Serenge, Quinter Adhiambo na Diana Onyango.

Nekesa alikuwa kipenzi cha mashabiki mwaka uliopita alipofunga mabao matatu dhidi ya Angola wakati wa mechi ya mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la wasichana wasiozidi umri wa miaka 20. Kenya ilipata ushindi wa 4-0 kabla ya kuondolewa Cameroon katika mchujo huo.

Safu ya viungo itakuwa na Velma Awuor, Brenda Awuor, Lorna Faith pamoja na Lindey Weey ambao pia ni wachezaji wa timu ya taifa ya wasiozidi umri wa miaka 15.

Halima Imbachi, Rebecca Odato na Susan Akoth pia wanatarajiwa kucheza katika safu hiyo.

Nahodha Elizebeth Ochaka, Claire Meries, Lorine Ilavonga, Jenevieve Mithel wategemewa katika safu ya ulinzi wakati kocha akiamua mmoja kati ya Ephy Awuor, Scovia Awuor na Velma Auma kuwa lango.

Kikosi cha Kenya: Makipa, Ephy Awuor, Scovia Awuor na Velma Auma.

Walinzi: Elizebeth Ochaka, Claire Meries, Lorine Ilavonga, Jenevieve Mithel, Christine Adhiambo, Judith Nandwa, Kimberly Akinyi, Dorcas Glenda na Sheryl Atieno.

Viungo: Velma Awuor, Brenda Awuor, Halima Imbachi, Rebecca Odato, Susan Akoth, Lorna Faith na Lindey Weey Atieno.
Washambulizi: Valerie Nekesa, Marion Serenge, Quinter Adhiambo na Diana Onyango.