Michezo

Junior Starlets yalenga kufuzu kwa Kombe la Dunia

June 8th, 2024 2 min read

Na TOTO AREGE

KIVUMBI kikali kinatarajiwa Jumapili saa tisa mchana wakati timu ya Junior Starlets ya Kenya itamenyana na Burundi katika mechi ya kwanza ya raundi ya nne ya mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake wenye umri chini ya miaka 17.

Burundi ndio wenyeji lakini mechi itachezewa katika uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mechi ya marudiano imepangwa Jumapili ijayo nchini Kenya katika uwanja ambao bado haujatangazwa.

Mshindi wa jumla katika mikondo yote miwili atafuzu kwa Kombe la Dunia ambalo litaandaliwa katika Jamhuri ya Dominika kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 3, 2024.

Kikosi cha Junior Starlets cha wachezaji 23 kiliondoka nchini mnamo Ijumaa saa kumi na mbili alasiri na kuwasili Ethiopia saa mbili usiku.

Mnamo Jumamosi, Kenya ilifanya mazoezi ya mwisho uwanjani Bikila kusubiri kujibwaga uwanjani kwa mechi yenyewe.

Kenya ilipenya hadi raundi ya nne na ya mwisho kwa kuiadhibu Ethiopia kwa jumla ya mabao 3-0 mwezi Mei 2024.

Timu ya Kenya haikucheza raundi ya kwanza na hivyo ikapewa tiketi ya moja kwa moja kucheza raundi ya pili ambapo, ilipangwa kucheza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo baadaye ilijiondoa kabla ya kucheza.

Kwa upande mwingine, Burundi pia ilipata nafasi ya moja kwa moja kucheza raundi ya pili na ilikutana na Botswana na kupata ushindi wa jumla wa 4-1, na kisha kushinda dhidi ya Djibouti kwa jumla ya mabao 24-0 katika raundi ya tatu.

Mashabiki wa Kenya wanaweza kuwa na matumaini kwa sababu Starlets haijawahi kupoteza dhidi ya Burundi.

Timu hizo mbili zilikutana mwaka wa 2019 wakati wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) nchini Uganda ambapo Kenya ilitandika Burundi 3-2 katika hatua ya makundi, lakini hatimaye kumaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano baada ya kufungwa 2-0 na Uganda katika nusu-fainali.

Kenya, chini ya kocha Mildred Cheche, inalenga kuweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kufuzu Kombe la Dunia. Ni muhimu kutambua kwamba hakuna timu ya soka kutoka nchini imewahi kufuzu kwa Kombe la Dunia.

“Kila mtu anatamani kushinda, na tumekuwa tukijitayarisha vizuri. Timu yoyote katika mechi hiyo inaweza kupata ushindi. Azma yetu kuu ni kufuzu kwa Kombe la Dunia,” akasema Cheche baada ya mazoezi Ijumaa katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi.

Burundi ikifunzwa na Daniella Niyibimenya, haikuweza kuandaa mechi za nyumbani kutokana na kukosa uwanja ulioidhinishwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Timu hiyo ilifika nchini Ethiopia mnamo Ijumaa jioni.

Katika mechi za raundi ya mwisho, Zambia itapambana na Morocco, huku Liberia ikikabiliana na Nigeria. Timu tatu kutoka bara Afrika zitakuwa miongoni mwa timu zitakazonogesha michuano ya Kombe la Dunia kwa Wanawake.