Michezo

Junior Stars U-15 yatwaa taji la FKF Elite League

October 1st, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya taifa kwa wasiozidi umri wa miaka 15 maarufu Junior Stars iliondoka katika uwanja wa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi kibabe baada ya kupiga Kamukunji All Stars magoli 3-2 katika fainali na kutawazwa mabingwa wa FKF Elite League.

Kikosi hicho kilijihakikishia kubeba ubingwa wa mapema baada ya

kucharaza Young United magoli 5-0 uwanjani MYSA Komarock, Nairobi na kufikisha alama 28 baada ya kucheza mechi 11. Kiungo wa Junior Stars, Kelvin Wangaya alituzwa mfungaji bora kwa kuitingia magoli tisa.

Katika baadhi ya matokeo ya mechi hizo, Junior Stars ililima Kariobangi Sharks goli 1-0, MYSA Talent ililazwa mabao 2-0 na Kamukunji All-Stars, Diamond ilipiga Uweza mabao 4-1, Ligi Ndogo ilibugizwa mabao 4-1 na Acakoro.

Nayo Vapour ilinyuka Centre of Excellence goli 1-0 huku Mukuru Talent ikikung’uta Young United mabao 3-0.

Kwenye kipute hicho kwa wasiozidi umri wa miaka 13, Kariobangi Sharks ilibeba taji hilo licha ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Mathare Youth Talent Academy (MYTA).

Kwenye patashika hiyo, Humphrey Omondi aliiweka Kariobangi Sharks kifua mbele alipocheka na wavu mara mbili dakika ya saba na 27.

Hata hivyo MYTA ilisawazisha kupitia Dominic Mureri na Brandon Muregi dakika ya 40 na 58 mtawalia. Kevin Wambua fowadi wa Kariobangi alitwaa tuzo ya mfungaji bora baada ya kucheka na wavu mara 18.