JURGEN NAMBEKA: Vijana watangamane na wanaowafaa msimu huu

JURGEN NAMBEKA: Vijana watangamane na wanaowafaa msimu huu

NA JURGEN NAMBEKA

LIKIZO za Desemba zimewadia baada ya mwaka kumalizika kwa kasi mno. Kila kijana nchini ameshuhudia mengi yaliyotokea tangu mwaka ulipoanza hadi sasa unaelekea kukamilika.

Sio Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 uliotupatia Rais mpya William Ruto, utambulisho wa naibu wa rais Rigathi Gachagua kama Riggy G, kuzama kwa meli ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na mengineyo.

Swali kuu kwa vijana ni je, mwaka unapokamilika ni yapi ya kufanya ufunge mwaka vyema?

Wakati wa likizo kwa wengi huwa ni muda wa kujiburudisha na kufurahia. Katika kampuni nyingi kutaandaliwa sherehe za kufunga mwaka, huku zingine zikipanga hata safari za kuwapeleka wafanyikazi nje kujivinjari.

Kama kijana, kuna mambo ambayo utafanikisha ukiwa na ujasiri. Kwa mfano, kabla ya sherehe, ni vigumu kuketi katika hafla moja na kuzungumza na bosi wako. Hii ni kwa sababu mara nyingi huwa ni wakati wa kazi. Rafiki mmoja alinipa ushauri ambao umeniongoza katika kipindi cha robo ya mwisho ya 2022.

Alinieleza: “Jitahidi uzungumze na wakubwa wako kazini ili ujifunze kutoka kwao na hata wakutambue.”

Kutokana na ushauri huu, ni wakati wa kujifunza mengi kwa wale walio na umri mkubwa kutuliko. Wahenga flani walikuwa wamenieleza nikialikwa katika karamu za kufunga mwaka na mabosi wangu wakuwepo nisijiachilie.

Ukifika katika sherehe kama hii iwapo itakuwepo, ni siku ambayo wakubwa wako watakuwa wanajiburudisha. Ni rahisi kufika katika meza yao na hata kuzungumza mawili matatu. Kwa hivyo usijifunge. Aidha, iwapo haujaajiriwa kazi, ni sawa kwani kuna njia nyingine ya kujijenga.

Vijana wengi hujifungia kwa kutaka kujitenga na wakubwa wao wakieleza kuwa wanafaa kuwa tu katika makundi hayo.

Changamoto yangu tunapofunga mwaka ni kujituma zaidi. Ni vyema kuamua kuzuru hoteli nzuri katika eneo lako na kupata hata kama ni sharubati ukiwa peke yako.

Usiandamane na watu unaowajua kwa kuwa, watakuzuia kutangamana na adinasi wapya katika ziara yako. Fika kwenye mkahawa mzuri ukiwa umependeza, ni kanakwamba ulikuwa umetoka nje kwa sherehe maalum.

Jifurahishe kadri ya uwezo wako na ukiweza, anzisha mazungumzo na wale utakaowakuta kule. Huenda mmoja wao atafurahia jinsi wewe kama kijana unajieleza. Labda hata akakuunganisha na watu au mashirika anayojua yatakusongeza mbele.

Likizo hii ni muda wa vijana kujituma, sio kwa kazi ila kwa kujifunza kutoka kwa wakuu wao katika ngazi zote, kikazi, kiumri ama kitajriba.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwapatie mafunzo mahasla watakaokopa...

KINYUA KING’ORI: Vikao vya Raila kutetea makamishna...

T L