Makala

JUSTUS THUKU: Kimuziki analenga kufikia wakali wa Bongo

June 19th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NI matumaini ya kila msanii kuona anafanya vizuri kisanaa na kukua kimuziki. Chipukizi yeyote huwa na maazimio ya kazi yake kuimarika na kuchota mashabiki wengi kote. Pia hutaka sana kuwashirikisha mastaa wakubwa ili kupata mpenyo wa kunawiri.

Justus Gichiri Thuku haachwi nyuma ingawa ndiyo ameanza kucheza ngoma anaamini atapiga hatua siku sijazo. ”Bila kujigamba sina budi kutaja kwamba nitatinga hadhi ya juu kimuziki ingawa katika utangulizi wangu wengi walidai sina kipaji,” anasema chipukizi huyu ambaye kimuziki nafahamika kama Achichiddeh.

Chipukizi anashukuru mwimbaji mtunzi wa fataki iliyotamba siyo haba ‘Welle welle’ Michael Kennedy Claver maarufu Naiboi awali akijulikana kama Rapdamu.

”Kusema siwezi kumweka katika kaburi la sahau ameibuka mzazi wangu katika muziki maana mapema mwaka huu alinitia motisha zaidi kurekodi nyimbo-audio ya kwanza ‘Bora uhai’,” alisema na kuongeza kuwa kwa sasa amezamia shughuli nzima kutoa video ya kibao hicho.

Nyimbo hiyo ambayo ametumia mtindo wa ‘kapuka’ imerekodiwa katika studio ya Pacho Records na prodyuza Jegede.

Kwenye nyimbo hiyo anasema licha ya binadamu kupitia pandashuka nyingi kimaisha uhai ni muhimu. Fataki hiyo aliitunga kwa kuzingatia maisha magumu ambayo amepitia akiwa mdogo ikiwamo kutoroka nyumbani kwa kipindi cha miezi saba baada ya kukosana na wazazi wake.

Chipukizi huyu aliyezaliwa katika mtaa wa Pumwani, Nairobi anakiri kuwa enzi zake akisoma alishiriki na kundi lililompoteza na kujipata akitumia mihadarati na kushiriki uhalifu mitaani. Picha/ John Kimwere

”Nakumbuka nilisoma kidato cha pili marafiki zangu walifanya niache shule kinyume na matakwa ya wazazi ingawa nao pia walikuwa wakilemewa kugharamia karo yangu.

“Licha ya hayo nashukuru yaliyopita si ndwele nilibahatika kubadilika na kutambua umuhimu wa kuisha maisha ya kawaida ndiyo maana nimezamia shughuli za kukuza talanta yangu katika kimuziki.”

Msanii huyu mwenye umri wa miaka 27 anasema amepania kukuza kipaji chake kufikia hadi ya waimbaji watajika nchini na Afrika Mashariki kwa jumla kama Nameless wa hapa Kenya na Proffessor Jay msanii wa bongo.

Kadhalika anadokeza kuwa analenga kufanya vizuri katika muziki na kuanzisha miradi mbali mbali kusaidia familia yake na vijana mitaani ambao mara nyingi hujikuta njiapanda kimaisha.

Kijana huyu anasema ingawa hajapiga hatua kubwa kulingana na matumaini yake amejitwika jukumu la kuzungumza na vijana mitaani hasa wanatumia mihadarati ili kukomesha mtindo maana anafahamu madhara yake.

Pia anatoa shukrani zake kwa ofisa mkuu wa Kinyago Youth and Sports Development (KYSD)Anthony Maina maarufu Coaches maana alikuwa mstari wa mbele kumpa mawaidha kuacha matumizi ya mihadarati na kushiriki matendo maovu mitaani.