Michezo

Juve ilinifukuza ili kupisha Ronaldo – Higuain

October 18th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Argentina anayesakatia timu ya AC Milan kwa mkopo Gonzalo Higuain amedai kwamba waliokuwa waajiri wake, mibabe wa soka ya Italia Juventus walimfukuza ili kupisha usajili wa nyota wa zamani wa Real Madrid Cristiano Ronaldo mwezi Julai mwaka 2018.

Higuain alijiunga na Juve kutoka Napoli mwaka wa 2016 na aliwafungia jumla ya mabao 40 katika ligi ya Serie A kwa muda wa misimu miwili aliyowawajibikia kabla ya kupigwa kibuhuti na uongozi wa Juve Agosti mwaka huu.

Hata hivyo hakuweza kuwatambisha Juve katika ligi ya Bara Uropa jinsi mashabiki wengi walivyodhania hali iliyoonekana kuchangia kutumwa kwake AC Milan kwa mkopo mwezi huo ili kuleta mwamko mpya chini ya ujio wa Ronaldo.

Ingawa hivyo mwanadimba huyo amesema kwamba hana kinyongo na Juve ila ilikuwa matamanio yake kusalia na klabu hiyo kwa muda wa miaka mingine zaidi ili aweze kuwadhihirishia kwamba angali moto wa kuotea mbali.

“Nilijitahidi na kucheza kwa kujituma sana nilipokuwa Juventus. Nilishinda tuzo kadhaa nao lakini baada ya Cristiano kusajiliwa mabingwa hao walinieleza kwamba hawakunihitaji tena na walikuwa wakitafuta mbinu ya kunipa uhamisho hadi AC Milan ambayo ninawachezea kwa mkopo sasa,”  akasema akizungumza na jarida la kispoti la Gazzetta dello Sport nchini Italia.

Nyota huyo hata hivyo amesema anayafurahia maisha katika timu yake mpya inayonolewa na mfalme wa soka ya Italia Genaro Gattuso huku akiapa kung’aa katika debi yake ya kwanza dhdi ya  majirani Inter Milan Jumamosi kwenye uga wa kihistoria wa Sansiro.

“Japo inasikitisha kwamba tupo katika nafasi ya 10 katika Serie A tunafaa kuwa miongoni mwa timu tatu bora. Kocha amezua ushirikiano wa kupigiwa mfano nasi kikosini na tunapenda mtindo wake wa uchezaji,” akaongeza.