Michezo

Dries Mertens aweka rekodi mpya Italia

June 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MFUMAJI Dries Mertens aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Napoli mnamo Jumamosi baada ya kufunga bao lililowabandua Inter Milan kwenye nusu-fainali za Coppa Italia msimu huu.

Napoli ambao ni mabingwa mara tano wa taji la Coppa Italia, walijibwaga ugani wakijivunia ushindi wa 1-0 kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza uliochezewa jijini Milan mnamo Februari 12. Bao hilo lilifumwa wavuni na Fabian Ruiz mbele ya zaidi ya mashabiki 60,000 waliojaza uwanja wa San Siro wakati huo.

Hata hivyo, matumaini yao ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya Inter ya kocha Antonio Conte yalitikiswa ghafla kwa bao la Christian Eriksen aliyefunga moja kwa moja kupitia mpira wa kona kunako dakika ya pili.

Mertens ambaye ni mzawa wa Ubelgiji, aliwasawazisha kunako dakika ya 41 na kuwasaidia Napoli kuwadengua Inter kwa jumla ya mabao 2-1. Bao lake hilo ambalo ni la 122 kambini mwa Napoli, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa na Lorenzo Insigne. Mertens kwa sasa amempiku Marek Hamsik wa Slovakia aliyekuwa akitoshana naye kwa idadi ya mabao hadi Napoli waliposhuka dimbani kuvaana na Inter.

Mertens ambaye mashabiki wa Napoli wamempagaza jina ‘Ciro’ kutokana na urefu wa uhusiano wake na kikosi hicho jijini Naples, kwa sasa anajivunia mabao saba zaidi kuliko nguli wa klabu hiyo, Diego Maradona.

Napoli walinyanyua ufalme wa Coppa Italia kwa mara ya mwisho mwaka wa 2014 na sasa watakutana na Juventus kwenye fainali itakayosakatwa ugani Olimpico, Roma mnamo Jumatano ya Juni 17, 2020.

Juventus ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la Coppa Italia, walitinga fainali ya kipute hicho kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya AC Milan kwenye mkondo wa pili jijini Turin mnamo Ijumaa usiku. Vikosi hivyo viliambulia sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliosakatiwa mjini Milan mnamo Februari 13.