Habari Mseto

Juve wapoteza mechi ya kwanza tangu 2018

August 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS ambao ni mabingwa wa Serie A, walipoteza mchuano wao wa kwanza kati ya 40 iliyopita katika uwanja wa nyumbani baada ya kupigwa 3-1 na Roma jijini Turin mnamo Agosti 1, 2020.

Miamba hao walinyanyua ufalme wa Serie A msimu huu kwa mara ya tisa mfululizo baada ya kutawala kilele cha jedwali kwa alama 83, moja pekee kuliko Inter Milan.

Ingawa Juventus walitawazwa mabingwa wakisalia na mechi mbili zaidi za kupiga msimu huu, waliibuka na ushindi katika michuano miwili pekee kati ya minane iliyopita.

Gonzalo Higuain aliwaweka Juventus uongozini kabla ya Nikola Kalinic kusawazisha kisha Diego Perotti kufunga mawili kwa upande wa Roma. Chini ya mkufunzi Antonio Conte, Inter walipepeta Atalanta 2-0 kupitia mabao ya Danilo D’Ambrosio na Ashley Young.

Hii ni mara ya kwanza tangu 2010-11 kwa Inter kukamilisha kampeni za Serie A katika nafasi ya pili na ni mara ya kwanza tangu 2001-02 kwa vikosi viwili vya kwanza kileleni mwa jedwali kutenganishwa na alama moja pekee.

Atalanta walishindwa kufunga bao kwa mara ya tatu mfululizo katika Serie A msimu huu. Hata hivyo, walifunga kampeni zao kwa mabao 98, hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya magoli kuwahi kufungwa kwenye Serie A katika msimu mmoja baada ya miaka 68.

Kwingineko, Zlatan Ibrahimovic, 38, aliweka historia ya kuwa mwanasoka mkongwe zaidi kuwahi kufunga mabao 10 katika Serie A alipowaongoza AC Milan kuwalaza Cagliari 3-0.

MATOKEO YA SERIE A (Agosti 1, 2020):

Juventus 1-3 Roma

Napoli 3-1 Lazio

Brescia 1-1 Sampdoria

Atalanta 0-2 Inter Milan

AC Milan 3-0 Cagliari