Michezo

Juve watenga Sh28 bilioni kumnunua Harry Kane

April 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS wamefichua azma ya kuweka mezani kima cha Sh28 bilioni na kujitwaliwa huduma za mvamizi wa Tottenham Hotspur, Harry Kane, 26.

Kufaulu kwa uhamisho huo kutamfanya Kane ambaye mzawa wa Uingereza kuwa mchezaji ghali zaidi baada ya Neymar Jr kuwahi kusajiliwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Juventus wanaanza kuyahemea maarifa ya Kane baada ya Real Madrid ya Uhispania kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania saini ya Kane kutokana na athari kubwa za virusi vya corona kwa hazina yao.

Awali, yalikuwa matarajio ya Daniel Levy ambaye ni mwenyekiti wa Tottenham kumshuhudia Kane akiingia katika sajili rasmi ya Real ambao wamekuwa washirika wao wa karibu kwenye soko la uhamisho wa wachezaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Ingawa Kane anakeshewa pia na Man-United, Levy ameshikilia kwamba si hulka yao kuwauza masupastaa wao kwa washindani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Katika matukio mawili chini ya mwongo mmoja uliopita, Real wamejinasia wachezaji wa haiba kubwa zaidi kutoka Tottenham. Mnamo 2012, Tottenham walikataa ofay a Man-United ya kumsajili kiungo raia wa Croatia Luka Modrid na badala yake wakahiari kumtoa kwa Real waliomsajili kwa kima cha Sh4.2 bilioni.

Mnamo 2013, Gareth Bale ambaye ni raia wa Wales alinunuliwa pia na Real kwa kima cha Sh11 bilioni. Fedha hizo zilimfanya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani kwa kipindi hicho.

Wakati huo, Bale ambaye kwa sasa anahusishwa na vikosi kadhaa nchini China, alikuwa akimezewa pakubwa na Man-United chini ya kocha wa sasa wa West Ham United, David Moyes.

Hadi walipoanza kumvizia Kane mwishoni mwa msimu jana, Real walikuwa pia wakihusishwa na uwezekano mkubwa wa kumsajili kiungo Christian Eriksen aliyehiari kujiunga na Inter Milan ya Italia baada ya kukatiza uhusiano wake na Tottenham mwanzoni mwa mwaka huu.

Hali ngumu ya kifedha kambini mwa Real imewachochea wasimamizi wa kikosi hicho cha Uhispania kuwashawishi masogora wao kukubali kupunguziwa mshahara kwa kati ya asilimia 10-20 hadi virusi vya corona vitakapodhibitiwa vilivyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Real kwa sasa wanapangia kuwatia mnadani wachezaji wanane ndipo iweze kujistawisha.

Mbali na kipa Alphonse Areola ambaye kwa sasa anawadakia Paris Saint-Germain (PSG) kwa mkopo, wachezaji wengine ambao wanatazamiwa kuagana na Real ni Bale, Lucas Vazquez, Mariano Diaz, Alvaro Odriozola, Nacho Fernandez, James Rodriguez na Isco ambaye kwa sasa ni kiazi moto kambini mwa Man-United, Arsenal, Chelsea, PSG, Borussia Dortmund na Bayern Munich.