Michezo

Juventus waanzisha mchakato wa kumsajili upya kiungo Paul Pogba

December 17th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wameanzisha mazungumzo na Mino Raiola ambaye ni wakala wa Paul Pogba, 27, wakijiandaa kumsajili tena kiungo huyo wa Manchester United.

Juventus ambao ni miamba wa soka ya Italia (Serie A), walimuuza Pogba mnamo 2016 kwa kima cha Sh12 bilioni na kwa sasa wako radhi kujivunia upya maarifa yake.

Kwa mujibu wa Raiola, Pogba ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia akivalia jezi za Ufaransa mnamo 2018, hafurahiio kabisa maisha yake kambini mwa Man-Unite na yuko radhi kubanduka uwanjani Old Trafford mnamo Januari 2021.

Raiola, 53, pia ni wakala wa wachezaji Zlatan Ibrahimovic, Erling Haaland na Matthijs de Ligt. Ajenti huyo amekuwa akimkosoa pakubwa kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa kutomwajibisha Pogba ipasavyo katika kikosi chake cha kwanza na badala yake kumweka benchi katika nyingi za mechi muhimu.

“Pogba hana furaha kabisa akichezea Man-United. Hawezi tena kujieleza jinsi anavyotaka na kwa namna anavyotarajiwa afanye,” akasema Raiola katika mahojiano yake na gazeti la Tuttosport nchini Italia.

“Itamlazimu abadilishe timu haraka iwezekanavyo. Inabidi abadilishe hewa. Ipo haja aondoke Man-United kwa sababu hajivunii kuwa katika zizi la Old Trafford,” akasema Raiola kwa kushikilia kwamba mteja wake hana nia yoyote ya kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Old Trafford kwa kutia saini kandarasi mpya na Man-United waliofichua azma ya kumpa kandarasi mpya mnamo Oktoba 2020.

“Mlango wa Juventus ni wazi kabisa kwa Pogba. Huenda huko ndiko anakorudi kwa kuwa anajivunia uhusiano mzuri na kikosi pamoja na wanasoka aliowahi kucheza nao katika klabu hiyo,” akaongeza Raiola katika kauli iliyoshadidiwa na mkurugenzi wa michezo kambini mwa Juventus, Fabio Paratici.

Pogba aliwahi kuagana na Man-United mnamo 2012 chini ya kocha Sir Alex Ferguson na kutua Juventus baada ya mkataba wake na miamba hao wa soka ya Uingereza kutamatika.

Akiwa Juventus, alisaidia wapambe hao wa soka kutwaa mataji manne ya Serie A na mawili ya Coppa Italia kwa mfululizo.